
SERIKALI ya Tanzania imepanga kulibadili eneo la bonde la mto Msimbazi kuwa eneo la uwekezaji na fursa mbalimbali ili kuondokana na changamoto zinazojitokeza katika mto huo.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Aprili 29, 2021 na naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Hassan Chande wakati akijibu swali la mbunge wa Kinondoni (CCM), Tarimba Abbas.
Tarimba alihoji ni lini Serikali itaanza ujenzi wa mto huo ambao umeainishwa katika Ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2020/25.
Akijibu swali hilo, Chande amesema Tamisemi inatekeleza mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project – DMDP) kwa mkopo nafuu wa Dola 300 milioni za Marekani kutoka Benki ya Dunia (WB).
Aidha, Serikali kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (DFID), inatekeleza programu ya Tanzania Urban Resilience Programme (TURP) ambayo imelenga kuzisaidia halmashauri na Serikali Kuu katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa kuanzia, programu itaanza kutatua changamoto zinazolikabili bonde la mto Msimbazi. Tayari DFID imeshatenga Dola 20 milioni za Marekani kwa ajili ya bonde hili,” amesema.
Amebainisha kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia mradi wa DMDP, imekubali mkopo wa nyongeza wa Dola 100 milioni za Marekani kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za bonde hilo.
Amesema Serikali imepanga kulibadili eneo la bonde kuwa la uwekezaji na fursa mbalimbali na tayari usanifu wa mradi huo umekamilika.
“Utekelezaji wa mradi utaanza baada ya kupata idhini ya Serikali kuhusu matumizi ya fedha hizo za mkopo kupitia Wizara ya Fedha na Mipango,” amesema.
Ameeleza kuwa ili kupunguza athari za mafuriko kwa sasa, kipande cha mto Msimbazi cha daraja la Jangwani kinafanyiwa usafi wa mara kwa mara na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).