
BINTI mmoja mkazi wa mkoa wa Geita, Anjelina Masumbuko mwenye umri wa miaka 17 anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kuiba mtoto mchanga.
Inadaiwa kuwa, Anjelina aliamua kuchukua uamuzi huo ili kunusuru ndoa yake baada ya mume wake kutaka mtoto mara kwa mara na yeye kushindwa kuzaa.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Henry Mwaibambe amesema kuwa Anjelina alikamatwa Aprili 22, 2021 akiwa na mtoto huyo na kubainisha kuwa Machi 12, 2021 saa 2 usiku, mtuhumiwa alimchukia mtoto wa Juliana Mlichades bila taarifa.
Inadaiwa baada ya Juliana kujifungua mtuhumiwa alijenga mazoea na mwanamke huyo akimsaidia shughuli mbalimbali na kwamba siku ya tukio, Juliana alimlaza mwanae ndani lakini aliporejea hakumkuta na alimtilia shaka mtuhumiwa huyo ambaye alikamatwa akiwa na mtoto huyo.
“Mtoto tulimpeleka hospitali akafanyiwa uchunguzi ana afya njema kabisa na amekabidhiwa kwa mama yake mzazi, Anjelina anaendelea mahojiano polisi na atafikishwa mahakamani wakati wowote,” amesema.