
WATUMIAJI wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania hii leo wanaweza kuingia katika mtandao wa Twitter bila kutumia mfumo wa usalama wa mtandao ‘Virtual Private Network’ (VPN) kama ilivyokuwa hapo awali.
Mtandao huo ambao ulikiuwa sehemu ya mitandao ya kijamii iliyofungwa miezi sita iliyopita ikiwa ni muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.
Mitandao mingine ilifunguliwa baada ya uchaguzi lakini mtandao wa Twitter uliendelea kufungwa hata baada ya uchaguzi.
Watu waliondelea kutumia Twitter kwa kipindi chote tangu wakati wa uchaguzi walilazimika kutumia njia ya mkato kwa kutumia programu tumishi za VPN.
Wakati Tanzania ilipochukua hatua hiyo mtandao wa Twitter uliandika kuwa “Tunashuhudia mtandao wetu kuminywa Tanzania”.
Twitter ilisema kufungwa kwa intaneti ni jambo lenye madhara na kuvunja haki za binadamu. Wakati ilipofungiwa, watumiaji wengi walihusisha suala hilo la zuio la mitandao na uchaguzi mkuu lakini mpaka sasa Serikali haikueleza kwa nini mitandao hiyo ilifungwa.