×

Muigizaji Maarufu wa Filamu Mzee Msiri Afariki Dunia

Muigizaji maarufu na mkongwe nchini Kenya aliyejizolea umaarufu zaidi katika kipindi cha runinga cha Pete akitumia jina la Mzee Msiri amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 62.

 

Mzee Msiri ambaye jina lake halisi ni Gillie Owino alifariki dunia jana Ijumaa Aprili 30, 2021 jioni saa chache baada ya kukimbizwa hospitalini jijini Nairobi ambako aliaga dunia.

 

Kulingana na taarifa kutoka kwa familia yake, Mzee Msiri amefariki kwa matatizo ya ugonjwa wa saratani. Mzee Msiri hakuonyesha dalili za kuwa mdhaifu hadi siku zake za mwisho ambazo pia alionekana akiwa studioni akiigiza.

 

Familia ilisema kwamba marehemu amekuwa akipokea matibabu kwa miaka kadhaa lakini hali yake ilidorora ghafla Alhamisim, Aprili 29 ambapo alikimbizwa hospitalini.

 

Madaktari walijaribu kadri ya uwezo wao kuyaokoa maisha yake lakini Mungu alikuwa ameshapanga mpango wake wa kumchukua. Mzee Msiri alikuwa mwandishi na mwongozaji wa filamu hasa katika maeneo ya mkoa wa Mombasa.

 

Mashabiki wake watamkosa sana hasa katika kipindi cha Pete ambacho hupeperushwa kwenye runinga ya Maisha Magic.

 

Kando na kuwa muigizaji, Mzee Msiri pia alikuwa mhasibu mstaafu. Mzee Msiri alijinyakulia tuzo kadhaa katika tasnia ya uigizaji moja ikiwemo ya Sanaa Awards aliyotuzwa mwaka wa 2018. Mashabiki kwenye mitandao ya kijamii wametuma rambi rambi zao kwa familia, jamaa na marafiki.

Leave a Comment