
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kulipa madeni yote inayodaiwa huku akiwaonya watumishi kwa kuzalisha madeni na kutengeneza madeni hewa.

Rais Samia amesema hayo wakati wa hotuba yake kwa wafanyakazi mbalimbali katika Kilele cha Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi Kitaifa ambazo zimefanyika Jijini Mwanza leo Mei 1, 2021 katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.

“Kuhusu suala la Watumishi wa darasa la saba waliositishiwa ajira najua wapo ambao hawajalipwa kwa kisingizio kuwa Serikali haijatoa mwongozo, naagiza Waajiri wote waliokuwa na Wafanyakazi wa aina hii wafanye kila linalowezekana wawalipe haki zao.
“Mimi ni mama, mama ni mlezi kuna msemo wa Kiswahili unasema maskini hapendi mwana, hata kama unataka mwanao apendeze, lakini huna uwezo wa kumfanya apendeze, ni kweli mishahara haijaongezwa miaka mingi, lakini kutokana na sababu mbalimbali, nimeshindwa kuongeza.

Katika bajeti ya mwaka 2021/22, tutapandisha vyeo watumishi 85,000 hadi 90,000, itatugharimu Sh.449 bilioni; Tutalipa malimbikizo ya watumishi Sh.60 bilioni mabadiliko ya muundo Sh.120 bilioni na tutaajiri watumishi 40,000 Sh.239 bilioni.

“Serikali imeongoza umri wa mtegemezi kwa mtoto kutoka miaka 18 hadi 21. Maamuzi haya, tutayajumuisha kwenye mabadiliko ya sheria. Natamani kuona mtu aliyestaafu anayelipwa mara moja na sio kuzungushwa muda mrefu.
“Kuhusu Bima ya Afya, Mtoto wa miaka 18 bado ni mtegemezi kwa Wazazi wake, tumeamua kuongeza umri wa Mtegemezi, tutatoka miaka 18 hadi 21 ambapo tunakusudia maamuzi haya kuyaweka kwenye marekebisho ya Sheria ya Bima ya Afya….. Kazi iendelee, tukaboreshe tija ili tukapandishe mishahara,” amesema Samia.