×

Vanessa Anaishi Kwenye Sayari Yake Ya Mapenzi

HEBU jiulize wewe mwenyewe kimyakimya hapo ulipo; kweli wewe ni pisi kali? Kama ndiyo, je, unakumbuka ni lini mwanaume wako alikununulia maua ya Valentine’s Day kama hii ya keshokutwa (Jumapili ya Februari 14) yenye gharama ya zaidi ya shilingi milioni moja za Kitanzania?

 

Basi taarifa ikufikie kwamba Vanessa Mdee almaarufu Vee Money au Cash Madam; yule aliyekuwa kinara wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania kabla ya kutundika daruga, anaishi kwenye sayari yake ya mapenzi pale Atlanta nchini Marekani.

Juzikati amenunuliwa maua mekundu ya msimu huu wa Valentine’s Day au mapenzi mubashara, yenye gharama ya zaidi ya shilingi milioni moja za Kitanzania kutoka kwa mchumba wake, Olurotimi Akinosho ‘Rotimi’; raia wa nchini Nigeria ambaye ni mwanamuziki, mwigizaji na mwanamitindo anayefanyia kazi zake hizo pale Marekani.

 

Baada ya miaka mingi ya kupambania penzi lake kwa msanii mwenzake wa Bongo Flava, Juma Mussa ‘Jux’, hatimaye mwaka 2018, Vanessa aliamua kunyoosha mikono juu kuashiria kusarenda na kushindwa kuendelea na penzi hilo lililodumu yapata miaka tisa. Hata hivyo, mashabiki wao walikuja kujua rasmi kwamba wawili hao wameachana mwaka 2019.

 

Hii ilikuwa ni baada ya Jux kuonekana na chombo kipya kutoka kule nchini Thailand kilichoitwa Nayika; kwa sasa hayupo nacho baada ya mambo kuwa ndivyo sivyo. Inaaminika bado Jux hajamsahau Vanessa ndiyo maana kila anapohojiwa huwa haachi kumtaja ‘eksi’ wake huyo.

Kwa kiasi f’lani, kitendo cha Jux kuwa na Nayika, kilimpa nafasi Vanessa naye kufungua moyo wake kwa mtu mwingine na huyo siyo mwingine, bali ni Rotimi pamoja na kwamba baadhi ya mashabiki walitamani kuendelea kumuona na Jux.

Wengine walikwenda mbali zaidi na kudai kwamba, huwenda Jux alimwacha Vanessa kwa sababu mrembo huyo alishindwa kumzaliwa mtoto, jambo ambalo jamaa huyo alilitamani kwa muda mrefu kutoka kwa Vanessa, lakini ni nani aliyewadanganya kwamba mtoto au watoto wanasaidia kuimarisha penzi?

 

Ni wanawake wangapi unawajua wamezalishwa na kuachwa wakilea watoto wenyewe?Ukweli ndiyo huo, lakini baada ya Jux kuachana na Nayika, wengi pia waliamini kwamba ulikuwa ni wakati muafaka wa kurejesha mpira kwa beki; yaani kurudi kwa Vanessa, lakini mambo hayakuwa mambo kwani mwanadada huyo aliripotiwa kukolea ile mbaya kwa Rotimi.

Ikawa hivyo, mwaka 2019, Vanessa akatangaza asmi kuwa kwenye mikono salama kabisa ya Rotimi ambaye aliyaponya majeraha yote ya Vanessa ya kuachana na Jux kiasi cha kuanza kunenepa.

 

Mwaka mmoja wa mapenzi shatashata, Vanessa na Rotimi mwishoni mwa mwaka jana (2020) walichumbiana kwa kuvishana pete ya uchumba na sasa, wengi wanasubiri hiyo ndoa ya kihistoria inayotarajiwa kufungwa mwaka huu (2021).

 

Hata hivyo, wakati tukielekea kwenye Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day) keshokutwa, Rotimi ameshafanya yake kwa Vanessa, mapema tu, amemkabidhi maua ya uaridi ya bei mbaya. Kuna mtaalam mmoja amesema maua hayo yana thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja za Kitanzania!

 

Kama alivyojipambanua kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Vanessa anaeleza furaha yake ya jinsi alivyopokea maua hayo kutoka kwa mtu sahihi aliyempa moyo wake na anayemfanya kuwa na furaha muda wote katika sayari yake ya mapenzi.

Ishu hiyo imeibua gumzo kama lote kwenye mitandao ya kijamii ambapo kila mmoja anasema lake; kwamba mtu huwezi kutumia pesa nyingi kiasi hicho kwa ajili ya kumnunulia mwanamke maua tu ilihali kuna jamii nyingi tu za Kiafrika zinakufa kwa njaa!Sasa mashabiki wa mwanadada huyo wamebaki kumzodoa tu Jux kwa kushindwa kumpetipeti Vanessa kama anavyofanya Rotimi. Yetuw macho, tusubiri yajayo kwani kuna mawili; yanaweza yakawa ni ya kurahisha au kuhuzunisha!

 

Leave a Comment