×

Matapeli Wamliza Lazaro Nyalandu

SIKU chache baada ya kurejea nyumbani –CCM, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Lazaro Nyalandu amedai kuna kundi la matapeli wanaotumia jina lake kutapeli watu mitandaoni.

 

Nyalandu ambaye alikuwa mmoja wa makada wa Chadema walioomba ridhaa ya kuteuliwa na chama hicho kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, alisema matapeli hao wanatumia jina lake kutapeli watu pesa.

 

Kupitia ukurasa wake wa Facebook Nyalandu aliandika, “Posts kama hizi ni za matapeli wa mtandaoni, wanatumia jina langu kutapeli watu. Mwisho wanawataka watume pesa wawatapeli. Tafadhali wapuuzeni”.

 

Posts alizozungumzia Nyalandu zilikuwa na picha yake na kuambatanishwa na maneno kuwa “Ninahitaji marafiki wawili wa ukweli kila wilaya kuna network ya kimaendeleo tunaiunda”.

 

Kutokana na ufafanuzi huo wa Nyalandu ambaye awali alikuwa mbunge wa Singida Kaskazini kupitia CCM kabla ya Oktoba 30 mwaka 2017 kuhamia Chadema kisha Aprili 30 mwaka huu akarejea CCM, alipongezwa na wafuasi wake katika mtandao huo.

 

Mmoja wa wafuasi hao Isaya Mbise alisema “Hilo Watanzania tunalielewa Mh Nyalanda hata usipate tabu, tunajua ni matapeli na majina makubwa yanayotumika sana ni wewe, Ridhiwan Kikwete na mengine ya akina mama Salma Kikwete n.k”.

NA GABRIEL MUSHI

Leave a Comment