
NI dhahiri kuwa sasa presha inapanda, inashuka kwa wakuu wa wilaya nchini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea na panga pangua ya safu mbalimbali za viongozi ikiwamo wakuu wa mikoa, wakurugenzi wa taasisi na makatibu tawala.
Tangua alipoingia madarakani Machi 19 mwaka huu, Rais Samia ambaye amerithi mikoba ya Rais John Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu, ameleta utofauti katika utendaji wake kwa kudhibiti siri mbalimbali zilizokuwa zinavuja ikilinganishwa na uongozi uliopita.
Yamkini watabiri au wachambuzi wa masuala ya kisiasa walikuwa wamefanikiwa kunusa mienendo ya Rais Magufuli ndio maana baadhi ya mambo waliyoyatarajia yalitokea kweli kama vile kuvuja kwa baadhi ya teuzi za viongozi.
Hata hivyo, mambo ni tofauti katika uongozi wa Rais Samia ambaye sasa anawaweka kiroho juuu wakuu wa wilaya ambao panga pangua inatarajiwa kuwakumba muda wowote kuanzia sasa.
Katika uteuzi wa Mei 29 mwaka huu Rais Samia alifanya uteuzi wa makatibu tawala wa mikoa 11, na kuwabadilisha vituo vya kazi makatibu tawala tisa huku wengine sita wakibaki katika vituo vyao vya kazi.
Sambamba na uteuzi wa makatibu tawala, Rais Samia alifanya uteuzi wa watendaji wawili wa mashirika ya umma ambapo alimteua William Erio kuwa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC) na Dk. John Mduma kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Kutokana na hali wachambuzi wa siasa wanaona kuwa sasa muda wa wakuu wa wilaya nao umefika hasa ikizingatiwa mmoja wao, Lengai ole Sabaya tayari ameshawekwa kando kutokana na tuhuma mbalimbali zilizokuwa zinamkabili.
Kupanda kwa joto la uteuzi katika nafasi mbalimbali, ni jambo ambalo liliwahi kuelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila ambaye awali alikuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya.
Chalamila alielezea namna hali inavyokuwa mbaya kwao kusubiri mabadiliko hayo hasa katika kipindi hiki ambacho uongozi mpya wa serikali umeshika hatamu.
“…,sisi wenyewe wakuu wa mikoa kwenye hii miezi miwili yaani ukilala usinzie hivi bahati mbaya ukiacha kiredio kinaimba imba ukisikia tu sauti ya mama Samia (Rais Suluhu Hassan) umeisha amka, mwenye salamu maria atasali pale huko ndiko ninakosema au umekufa hujielewi,” alisema Chalamila wakati akiwaeleza watumishi wa mkoa wa Mwanza kabla ya kuhamishwa mkoani humo.
NA GABRIEL MUSHI