
STAA wa muziki wa kizazi kipya kutoka Zambia, Jay Rox ameingia studio na Mbongo Fleva, Jux na mwenzake Kenz Ville Marley, kuandaa ngoma mpya, ‘Changanya’ ambayo imeimbwa kwa kuchanganya lugha mbili, Kiswahili na Kinyanja.
Ngoma hiyo ni mchanganyiko wa tamaduni za Zambia, Tanzania na Afrika Mashariki ambapo tayari imeanza kupokelewa vizuri, gumzo kubwa likiwa ni mashairi yake yenye hisia za mchanganyiko wa mambo mbalimbali katika uhusiano wa kimapenzi.
Changanya ina mchanganyiko wa fleva za Zambia, Zed Beats na Bongofleva ambapo kazi kubwa imefanywa na maprodyuza wawili, Kenz na Beingz ambao ndiyo waliohusika kuandaa ngoma ya Distance Remix ya mkali Rayvanny na AY.
Kwa upande wa video ya wimbo huo, Dairekta Jordan Hoechli amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha inakuwa na ubora wa kimataifa, akitengeneza ladha nzuri za wasanii wote walioshiriki.
“Kufanya kazi na Jux ilikuwa ni zaidi ya muunganiko wa studio, tumefanya kazi kubwa ambayo naamini itakwenda kupanua wigo wa biashara yetu ya muziki. Nimefurahishwa na namna Jux alivyofanya kazi kubwa,” amesema Jay na kuongeza:
“Mimi na Jux tuna vitu vingi vinavyofanana. Mbali na kuwa mwanamuziki, Jux ana akili ya biashara na ndiyo maana amefungua lebo yake ya mavazi, African Boy! Mimi pia ninayo lebo yangu ya mavazi na viatu ambayo nafanya kazi kubwa ya kui-push ijulikane.”
Akiwa na ndoto za kuupa nguvu muziki wa Zambia na kuufanya ujulikane nje ya mipaka, kwa kipindi kirefu Jay Rox amekuwa akifanya kazi kubwa ya kutengeneza jina lake kwa kufanya ngoma na wasanii wakubwa huku akijizolea mashabiki lukuki kwenye mitandao ya kijamii.
“Nataka kuliteka pia soko la muziki katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” alihitimisha Jay.