
MAHAKAMA kuu ya Tanzania kanda ya Dar es salaam imetengua uamuzi wa kamati ya maadili ya mawakili wa kumfutia moja kwa moja uwakili mwanasheria Fatma Karume.
Pamoja na kutengua uamuzi huo, Mahakama hiyo imeagiza uamuzi huo uliotokana na malalamiko yaliyowasilishwa na mwanasheria mkuu wa serikali yarejeshwe kwenye Kamati hiyo ya Maadili na mwanasheria huyo apewe nafasi ya kujitetea.
Hata hivyo, uamuzi huo haimaanishi amerejeshewa uwakili wake uliofutwa awali, isipokuwa anapaswa kwenda mbele ya kamati ya maadili ili kujitetea.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter Fatma maarufu kama Shangazi ameandika hivi; “Jopo la Majaji ya Mahakama Kuu limechukua chini ya miezi 9 kufikia maamuzi ya kusema Maamuzi ya Advocate’s Committee ni haramu. Kwa hilo ninashukuru.”
Septemba 20, mwaka 2019, Fatma alisimamishwa uwakili na Mahakama Kuu kwa madai ya kuishambulia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kufikishwa mbele ya Kamati ya maadili ya mawakili ambayo nayo ilimkuta na hatia ya kukiuka maadili ya Uwakili na kuamuru jina lake (Namba 848) kuondolewa katika orodha ya mawakili.