MKURUGENZI Mkuu wa Tamasha la filamu za Nchi za Majahazi (Zanzibar International Film Festival-ZIFF ) Profesa Martin Mhando ameeleza kuwa, filamu za kutoka Bara la Afrika ikiwemo Tanzania, zina nafasi kubwa ya kufanya vizuri ndani ya Afrika na hata Bara la Ulaya zikipewa nafasi ya kuonekana kwenye majukwaa makubwa ya filamu.
Prof. Mhando amesema hayo leo 15 Julai wakati wa utambulisho wa ZIFF 2021 kwa Waandishi wa Habari tukio lililofanyika Alliance Française Dar es Salaam wakati wa kujibu maswali kwa Wanahabari juu ya uwepo wa tamasha hilo pamoja na faida za mchango wa Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Ulaya (European Union) ambao ni moja ya wadhanini wa tamasha mwaka huu.
Aidha, katika swali hilo Wanahabari walitaka kufahamu mchango wa ZIFF katika kuzifikisha mbali filamu za Kiafrika katika Bara la Ulaya.
“Jukwaa la ZIFF ni miongoni mwa majukwaa makubwa ya filamu Tanzania na Bara la Afrika.
Ndio maana kila mwaka tunapokea filamu nyingi kutoka mataifa yote duniani.
….mwaka huu filamu zaidi ya 200 zilitumwa kuombwa kuchaguliwa lakini tukafanikiwa kuzichagua ambazo ni bora zaidi 65.” Alisema Prof. Mhando.
Ambapo ameongeza kuwa, thamani ya tuzo za ZIFF ni kubwa hivyo kwa sasa wanaangalia kuongeza fedha ‘kifuta jasho’ kwa washindi.
“Ukishinda tuzo za ZIFF ni nafasi ya kupata kuonekana zaidi katika majukwaa makubwa ya filamu duniani ikiwemo Nchi za Ulaya ambapo kupitia wadau wao kama Ujerumani wanakuwa na nafasi ya kuonyesha filamu zote zilizoshinda tuzo ZIFF.
Lakini awali huko nyuma mbali ya tuzo tulikuwa pia tukitoa kiasi cha fedha kidogo ila kwa mwaka huu tunataka kukiongeza angalau kinone kutoka Tsh. 500,000 na kuongeza ilikusaidia mshindi afurahie matunda yake”. Alisema Prof. Mhando.
Katika hatua nyingine Prof. Mhando amewapongeza wadhamini wote waliojitikeza kulishika mkono hadi kufanyika kwake mwaka huu.
“Wadhamini wa ndani na wa nje kipindi hiki ni kigumu kuwapata. Tunashukuru waliojitikeza ZIFF2021 mwaka huu tumelenga zaidi Wanawake na filamu.
Prof. Mhando amezitaja filamu hizo 65 ikiwemo za Tanzania ni pamoja na; Binti, Decision, Dream, Murasi, Neema, Nyara, Salama, Shujaa wetu, Simba, Timela, Usiku mrefu, Nyundo, Kijiji changu huku kwa Animation ama katuni ni Mbuland na Mozizi.
Filamu zingine ni pamoja na; A fool God, A trip of Heaven, Adam, Al sit, Carton rouge, Catch out, Coffee place, Days of Cannibalism, Deliveries, Bablinga, Bottleneck, Breaking ground, Dream child, Banyalga, Dreams of trains, Excuse, Fakh (The Trap), Heart attack, If Objects could talk na Interstate 8.
Pia zipo Itswa, Joy’s Garden, Letter to my child, Mission to rescue, Morning after, My culture my music, Naisula, Njaa, Nursery rhymes, Revolution, Shaina, Sikelela tapes, Softie, Sororal, Tales of the Accidental city, Tazara stories, The blind date, The Colonels stray, The fever, The Grandpa, The Handyaman, The Heartbeat, The Letter, To Zanzibar, Underestimated Villain, Walled Citizen na Why U hate.
Katika mkutano huo, pia Wanahabari walishuhudia filamu ya MBULAND yenye mfumo wa Kikaragosi iliyokuwa na ujumbe wa mapambamo ya vita dhidi ya ugonjwa wa malaria.
