
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kufadhili fedha kwa ajili ya kutekeleza vitendo vya kigaidi.
Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali, Tulimanjwa Majigo amesema kuwa mshtakiwa Mbowe amefikishwa mahakamani na kuunganishwa na washtakiwa wengine watatu waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka mengine yote ya ugaidi wanayodaiwa kutenda mnamo mwaka 2020.
Kesi hiyo imesomwa mbele ya Hakimu Mkazi, Thomas Simba ambapo katika kosa la kwanza Mbowe anadaiwa kupanga njama za kutenda makosa ya kigaidi kati ya Mei na Agosti 2020 akiwa katika Hoteli ya Aishi Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni pamoja na kuwasha vituo vya mafuta na kwenye mikusanyiko ya hadhara kwa kutumia vilipuzi.
Katika kosa la pili Mbowe anadaiwa kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi kinyume cha sheria ya makosa ya ugaidi na kesi hiyo imeahirishwa mbele ya Hakimu Thomas Simba hadi Agosti 5, 2021 na upelelezi umekamilika kwa ajili ya kupeleka nyaraka Mahakama Kuu.



