
NI rasmi sasa uongozi wa Simba unatarajia kuanza rasmi programu za mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, Agosti 8, mwaka huu ambapo watafungua msimu na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.
Ligi Kuu msimu ujao inatarajiwa kuanza rasmi kutimua vumbi mwezi ujao na kwa kawaida kuendana na kanuni mchezo huo wa Ngao ya Jamii huwa maalum kwa ufunguzi wa ligi kwa msimu husika.
Mchezo huo huwakutanisha bingwa wa Ligi Kuu Bara, dhidi ya bingwa wa Kombe la Shirikisho au timu itakayokuwa mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho, kama bingwa wa ligi ndiyo bingwa wa FA, hivyo kwa msimu unaotarajiwa kuanza Simba na Yanga ndizo zitakuwa na kibarua hicho.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Meneja wa kikosi cha Simba, Patrick Rweyemamu alisema: “Kikosi chetu kinatarajiwa kurejea kambini kuanzia Agosti 8, mwaka huu kwa ajili ya kuanza kujiandaa na michuano mbalimbali tutakayoshiriki msimu ujao.
“Tunataka kuwa na maandalizi mazuri ya msimu ili kuendelea pale tulipoishia msimu uliyopita, kwa kufanya vizuri zaidi kwenye michuano ya msimu ujao.”
Inaelezwa kuwa wachezaji wapya wote wa Simba watakuwepo mazoezini siku hiyo, hivyo mashabiki wanaotaka kufahamu timu hiyo ambayo imetwaa makombe yote makubwa msimu huu imemsajili nani itawaona.
JOEL THOMAS, Dar es Salaam