
WANANCHI mpo? Leo huenda ikawa ni siku ya furaha tena kwenu baada ya yule straika aliyeondoka mkiwa bado mnamhitaji, Heritier Makambo, kutarajiwa kutua kwenye ardhi ya Bongo.
Viongozi waandamizi wa Yanga wamethibitisha kuwa staa huyo raia wa DR Congo, ambaye alikuwa anakipiga kwenye kikosi cha Horoya ya Guinea, alishatumiwa tiketi na alipewa siku tatu, jana Jumapili, leo Jumatatu na kesho Jumanne kutua Tanzania.
Makambo anakuja Tanzania ikiwa wikiendi iliyopita tu Wanayanga wameshuhudia straika mwingine kutoka AS Vita ya DR Congo, Fiston Mayele, na kiungo mshambuliaji, Jimmy Julio Ukonde wakitua kuja kuanza kazi ya kuitumikia Yanga.
Kiongozi mmoja maarufu wa Yanga aliliambia Championi Jumatatu kuwa: “Kuanzia leo Jumapili (jana), kesho Jumatatu (leo) au Jumanne huenda Makambo akatua Tanzania kuja kumalizana na sisi, kwa sababu tiketi alishatumiwa na ilibidi aje pamoja na Mayele lakini akapata dharura. Kwa hiyo bila shaka hizi siku mbili atatua.”
Championi lilimtafuta Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro ili kujua ukweli wa taarifa hizo ambapo alisema: “Nafikiri inaweza kuwa kweli, kwa sababu kuna watu wanasimamia hayo mambo kwa sasa mimi nipo bize na Kagame Cup.”
Makambo alicheza msimu mmoja Yanga, 2018-19 na kufunga mabao 17 ya ligi, kisha mwisho wa msimu akatimka na kwenda Guinea kujiunga na Horoya ambayo amevunja nayo mkataba msimu huu.
ISSA LIPONDA, Dar