×

Bwege: Naunga Mkono Tozo, Mwanasiasa Haogopi Kufungwa Wala Kufa – Video

 

MBUNGE Mstaafu wa Jimbo la Kilwa Kusini, Suleiman Bungara maarufu kwa jina la Bwege amesema yeye anaunga mkono tozo ya miamala ya simu iliyopitishwa na Bunge kuanza kufanya kazi hivi karibuni kwani makusanyo yatasaidia kutanua wigo wa kupeleka huduma muhimu kwa wananchi na kwa haraka.

 

Bwege amesema hayo leo Alhamisi, Agosti 5, 2021 wakati akihojiwa na kipindi cha Front page cha Global Radio huku akishauri kuwa tozo hizo zinatakiwa zipunguzwe ili wananchi waweze kulipia bila malalamiko.

 

“Hata hii katiba tuliyo nayo kuna mambo ambayo hayasimamiwi vizuri, tukipata katiba mpya tutajua sasa tumesema hiki, huyu akienda kinyume tutajua namna ya kupambana naye, lakini katiba sio suluhisho kwa nchi ninavyoiona.

 

“Sisi hatukuharibu mchakato wa Katiba Mpya, mawazo ya wananchi ambayo ndio waliotutuma hayakuwa yakizingatiwa, tukaamua kutoka lakini haikusababisha Ikama ya Bunge kutoendelea, Bunge liliendelea na wakapitisha, ikafika hatua ya kupiga kura.

 

“Sisi ni wanansiasa, wanasiasa ni wawakilishi wa wananchi, hata Mwl. Nyerere aliomba uhuru kupitia chama cha siasa, aliyeanzisha hoja ya Katika Mpya ni Rais Jakaya Kikwete (mstaafu) na CCM kwa ajili ya wananchi, huwezi kuwatofautisha wananchi na siasa.

 

“Tozo ya Miamala ya Simu naunga mkono lakini kubwa, lile jambo ni muhimu tozo ipunguzwe tu. Iwekwe kwenye mfuko maalum na kila mwezi watuambie wamekusanya Shilingi ngapi na kiasi gani wamepeleka kwenye huduma eneo gani kama ni Kilwa.

 

“Katika wakati wa ubunge wangu jambo ambalo siwezi kulisahau ni mambo ya utekaji, kule kwangu Kilwa kuna watu walipigwa risasi msikitini, nilisema Bungeni, niliandika Barua kwa waziri Mkuu, kwa Mhe. Magufuli na sasa nimeandika kwa Rais Samia.

 

“Mwanasiasa haogopi kufungwa wala kufa sababu yeye anataka haki itendeke, nilivyoona Prof. Lipumba ameungana na watu naamini hawapo sawa nikaona huyu hataki haki, anataka mkwanja tu, nikajua CUF itashuka tu, nikaenda ACT-Wazalendo.

 

“Chadema inaeleweka Bara, wanapambania haki, hiki anachofanyiwa Freeman Mbowe ni kukipaisha Chadema. Usione tupo kimya, siasa ni busara, ukitaka kumuua nyoka aliyeko chumbani mwako, ingia chumbani upambane naye, na si vinginevyo.

 

“ACT Wazalendo tutachukua Zanzibar, huku Bara tutakuwa wa pili, tutawapiku Chadema sababu sisi tunapambana nje na ndani wao wanapambana ndani tu. Uchaguzi wa Konde (Pemba – Zanzibar) isingekuwa kupambana nje na ndani yule jamaa asingejiuzulu.

 

“Nimesema tunapambana nje na ndani, ndio maana yule kaambiwa jiuzulu (aliyekuwa Mbunge Mteule wa CCM Jimbo la Konde, Sheha Mpeka Faki), bila hivyo kusingekuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, sisi hatuna haraka, tunasubiri kuanzisha dude.

 

“Chadema wanadai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi, sisi ACT Wazalendo tunataka tuanze mikutano ya hadhara, jino kwa jino hiyo. Katiba hii hii iliyopo iheshimiwe, nampenda sana Mama Samia, ninamuelewa sana na ninamkubali vilevile, lakini ninamuomba akae na wanasiasa, sababu hawa wanasiasa wanaweza kuiacha nchi salama ama wakaiharibu,” amesema Bungara (Bwege).

Leave a Comment