
Funzo kubwa analowapa vijana wenzake ni kuamini na kuweka juhudi katika unachokifanya bila kujali unakutana na changamoto kiasi gani! Huyu ni Mussa Mohamed Bakari, maarufu kwa jina la Jabulant, mpigapicha wa mwanamuziki mkubwa Bongo, Rajab Abdul ‘Harmonize’.
Kabla ya kuanza kushika kamera, Jabu alikuwa mchoraji mzuri, kipaji kilichomfanya baba yake apambane kufa kupona ili mwanaye atimize ndoto za kuwa mchoraji mkubwa duniani lakini kwa bahati mbaya baba yake alifariki kabla hata robo ya ndoto ya mwanaye haijatimia.Na hapo ndipo maisha ya Jabu yalipoanza kubadilika na akaanza kujifunza kupiga picha mtaani hadi akawa hodari wa kupiga picha kali zenye ubunifu wa hali ya juu.

Mpaka sasa Jabulant ameshafika katika nchi mbalimbali kupitia kamera ikiwemo Ghana, Australia, Nigeria n.k ambayo aliamua kuipa heshima na kuwa nayo ‘serious’ tangu akiwa anaishi maisha ya kuungaunga maeneo ya Gongo La Mboto, Ukonga jijini Dar kabla ya kukutana na Konde Boy mwaka 2018.
Siri kubwa ya Jabulant kutoboa ni kwamba aliamini kwamba kamera ni kazi na ndio maana aliiheshimu na kuipa thamani kubwa. Jabulant alipokutana tu na Harmonize, alifungua ukurasa mpya wa maisha yake kwa kuanza kumpiga picha na hata kumshuti video za nyimbo zake kadhaa.

Maisha yake yamebadilika, akikusimulia ni kama unasikiliza ule wimbo wa bosi wake wa ‘Never Give Up’ yaani sasa hivi Jabulant yupo vizuri, uhakika wa milo mitatu kwa siku anao.
Watu wengi wamekuwa wakimshindanisha yeye na mpigapicha wa Diamond anayefahamika kwa jina la Lukamba, ila kwa upande wake amesema sio kitu kibaya na imekuwa ikimpa changamoto ya kuendelea kufanya vizuri zaidi.
Kupitia Jabulant, vijana wana jambo kubwa la kujifunza, somo la kuipa thamani kazi yako ni kubwa mno, na kwa sasa ukitaja miongoni mwa mastaa wakubwa wenye picha kali mtandaoni huwezi kuacha kumtaja Harmonize, na hapo lazima utamsifia mwanaume aliyeko nyuma ya kamera ambaye si mwingine ni Jabulant.