
JUMLA ya wanafunzi 249 wamedahiliwa kuanza masomo ya kidato cha tano kwa mwaka wa masomo 2021/2022 katika shule za Bugando na Kamena mkoani Geita ikiwa ni mwendelezo wa mipango ya Kampuni ya Geita Gold Mine Ltd. – GGML kuboresha mazingira ya elimu mkoani humo.
Shule hizo ambazo ni za Serikali zilijengwa na kampuni hiyo ya GGML kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Geita kwa gharama ya Sh milioni 287.5 kupitia mfuko wa uwajibika kwa jamii wa kampuni hiyo.
Akizungumzia udahili huo Kaimu Afisa Elimu, Taaluma wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Navaya Alphonce alisema tangazo la kuanza kupokea wanafunzi hao kwa shule hizo limepokelewa kwa furaha na wananchi wa mkoa wa Geita na wadau wote ikiwemo GGML.
Alphonce alisema, “udahili wa wanafunzi ni mafanikio makubwa kwa sekta ya elimu nchini na sasa tayari wanafunzi tayari wameanza kuhudhuria masomo vyema.
“Tunaamini kwamba Kamena na Bugando ni mifano mizuri ya jinsi shule inavyopaswa kuwa kwa sababu shule zote zina mazingira yanayomfaa mwanafunzi kusoma na tuna imani tutashika nafasi ya juu zaidi na kushindana kimasomo na shule zingine zinazoongoza nchini.
“Ingawa tuna mihula miwili katika mwaka wa masomo, kati ya wanafunzi 249 katika shule zote mbili hatujapokea taarifa kutoka kwa mzazi yeyote anayeomba kumhamisha mtoto wake kutoka katika shule hizi. Huu ni uthibitisho kwa walimu na wafanyikazi wote wa shule hizi kujitolea kufundisha kwa bidii ili kusaidia wanafunzi hawa wa Kamena na Bugando kufanya vizuri,” alisema.
Aliongeza kuwa shule zote mbili zina nafasi nzuri ya kuvutia kwa wanafunzi wanaopenda masomo ya sanaa na sayansi na kuna matumaini kwamba Shule za Sekondari za Bugando na Kamena zitatoa wahitimu wa baadaye ambao watakua kitaaluma na kuwa watalaam bora katika tasnia mbalimbali hapa nchini.
Alisema shule hizo zilijengwa kwa bajeti ya pamoja ya Sh milioni 287.5 na kuungwa mkono na GGML na Halmashauri ya Wilaya ya Geita chini ya mpango wa Uwajibikaji wa Jamii kwa Jamii wa 2018.
Tangu marekebisho ya Sheria ya Madini mnamo 2017 yafanyike, GGML imetekeleza miradi kadhaa ya kimkakati katika mkoa wa Geita kupitia mipango ambayo inakusudia kuboresha maisha ya jamii inayozunguka mgodi huo.
NA MWANDISHI WETU