
BAADHI ya majirani wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa wameeleza namna walivyoguswa na kifo cha kiongozi huyo kwani alikuwa karibu nao kwenya mambo mengi.
Juliana Nyambuya (71) alisema yeye alifika eneo la Picha ya Ndege tangu 1983 na kwamba kiongozi huyo ambaye pia alikuwa Mbunge wa Ushetu alikwenda kununua eneo na akajenga makazi yake.
Nyambuya alisema aliishi na Kwandikwa kama ndugu yake na alikuwa akimsaidia kwa hali na mali pamoja na kumuwezesha kujenga chumba na sebule.
“Kwa kweli alikuwa ni msaada mkubwa kwangu, amenisaidia mambo mengi hata hii nyumba chumba na sebule amenisaidia kujenga yeye ijapokuwa bado haijaisha kuweka milango na madirisha, hizi ni jitahada zake,” alisema na kuongeza:
“Kwa kweli sina la kusema nilikuwa nasubiri akitoka hospitali anisaidie kuna mtoto wa mwanangu amefaulu kwenda kidato cha tano lakini tumeshindwa kumpeleka nilipanga nimuombe anisaidie baadhi ya vitu ili mjukuu wangu aende shule.”
Diwani wa Kata ya Picha ya Ndege, Karim Mtambo alisema Kwandikwa alikuwa na ushirikiano mkubwa na majirani zake. “Katika kumuenzi tutakaa ili barabara ya kuelekea kwake tuipe jina la Kwandikwa ambapo kwa sasa inaitwa Barabara ya Waziri,” alisema.
Alisema hivi karibuni walipokuwa kwenye mkutano kuhusu soko la Picha ya Ndege, Kwandikwa alitoa ushauri na akasema baadhi ya mambo angeyafanyia kazi ili magari madogo ya abiria (daladala) yapite kwenye eneo la soko.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Picha ya Ndege, Joseph Zambo ambaye ni jirani na marehemu alisema Kwandikwa alikuwa akisaidia shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye mtaa huo.
Rais Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuongoza waombolezaji kuuaga mwili wa marehemu katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam. Baada ya kuagwa Dar es Salaam utapelekwa nyumbani kwake Kibaha na Agosti 7 utapelekwa Kahama na baadaye nyumbani kwake katika kijiji cha Butibu, Ushetu kwa ajili ya maziko Agosti 9.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juzi aliishukuru familia kwa kuridhia Kwandikwa azikwe Jumatatu ijayo ili kuwapa nafasi ya waombolezaji wakiwemo wabunge wasafiri kutoka waliko wakashiriki kutoa heshima za mwisho na maziko.