
HABARI mpya ni kwamba, aliyekuwa Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck, ameushinikiza uongozi wa timu yake ya FAR Rabat ya nchini Morocco, kutenga shilingi bilioni 1.8, kwa ajili ya kumalizana na kiungo mnyumbulifu wa Simba, Clatous Chama raia wa Zambia.
Bodi ya Wakurugenzi ya Simba chini ya Mwenyekiti, Mohamed Dewji, tayari imeshakutana kujadili juu ya suala hilo, ambapo wengi wamekubaliana na ofa hiyo na kuwa tayari kumuachia.
Chanzo chetu kutoka ndani ya Simba, kimelinyetishia Spoti Xtra kwamba, uwezekano wa Chama kuondoka Simba ni mkubwa sana.“Tayari FAR Rabat imewasilisha ofa yao ya kwanza shilingi bilioni 1.8, fedha ambazo ukilinganisha na thamani ya Chama, kuna uwezakano mkubwa kabisa Simba wakamuachia.
“Waarabu hao wameonekana kuwa siriazi na Chama ikiwa ni baada ya kurudi kwa viongozi wa Simba kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kumsajili nyota huyo.“
Anayepambania usajili huo ni aliyekuwa kocha wa Simba, Sven ambaye ameonekana kumuhitaji Chama katika kukisuka kikosi chake kwa msimu ujao.
“Hivyo kama mazungumzo yakienda vizuri, basi huenda Chama akaondoka Simba katika msimu ujao na kutafuta mbadala wake kama ilivyokuwa kwa Luis Miquissone anayeuzwa Al Ahly ambaye mbadala wake ni Peter Banda,” alisema mtoa taarifa huyo.
Hivyo basi, kama mazungumzo yakienda vizuri, basi kiungo huyo atauzwa na kwenda kuungana na Sven ambaye walikuwa wote kuanzia Desemba 12, 2019 hadi Januari 7, 2021.Chama juzi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii alisema kuwa: “Kama ofa nzuri ikiletwa Simba, basi nitaondoka kama ilivyokuwa kwa Luis.”
STORI NA MUSA MATEJA NA WILBERT MOLANDI, Dar