
WANANCHI nchini Zambia leo Agosti 12, wanapiga kura katika uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa.
Zoezi la upigaji kura limeanza mapema asubuhi ambapo vituo zaidi ya 12,000 vya kupigia kura vilifunguliwa saa 12 asubuhi kwa saa za Zambia ambapo vitafungwa saa 10 jioni.
Uchaguzi huo unahusisha wagombea 16 wa nafasi ya urais wa nchi hiyo ambapo Rais aliyepo madarakani Edgar Lungu anawania kuchaguliwa kwa muhula wa pili kupitia chama chake cha Patriotic Front (PF), huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea Hakainde Hichilema kupitia United Party for National Development (UPND).
Hichilema ambaye ni mfanyabiashara mkubwa nchini Zambia anawania nafasi ya urais kwa mara ya sita sasa, ambapo anaungwa mkono na vyama vingine 10 vya siasa.
Tume ya uchaguzi nchini humo imesema matokeo ya uchaguzi huo yatatangazwa ndani ya masaa 72 baada ya kukamilika kwa upigaji wa kura, ambapo mshindi wa nafasi ya urais atapaswa kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizohesabiwa.