×

Polisi Yasema Waliouawa Wafikia Wanne – Video

WATU wanne wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa katika tukio la kurushiana risasi baada ya mtu mmoja ambaye hajafahamika kuwavamia polisi, kuwafyatulia risasi na kuwaua kisha kuchukua silaha katika maeneo ya daraja la Salenda karibu na Ubalozi wa Ufaransa, jijini Dar es Salaam.

 

Tukio hilo la aina lililozua taharuki miongoni mwa wananchi limetokea leo Jumatano, Agosti 25, 2021 baada ya mtu huyo kufyatua hewani risasi huku akisikika akisema kuwa anawatafuta polisi. Akizungumza na wanahabari katika eneo la tukio, Mkuu wa Oparesheni Maalum za Kipolisi Liberatus Sabas amesema;

 

“Leo Agosti 25, 2021 tumekutwa na tukio la kiharifu, mtu mmoja ambaye hajafahamika alifika eneo ambapo walikuwepo askari wetu wakiwa kazini, akachomoa bastola na kuanza kuwashambulia kwa risasi na kusababisha vifo vya askari watatu ambapo askari polisi ni wawili na mmoja wa Kampuni ya SGA.

 

“Alichukua silaha na kuanza kurusha risasi hovyo, akaelekea karibu na Ubalozi wa Ufaransa huku akirusha risasi, amejeruhi watu sita. Askari wetu wamemdhibiti na kumuua. Hivyo jumla ya watu wanne wameuawa kutokana na tukio hilo.

 

“Kwa sasa ni mapema sana kujua nia yake ya kufanya hivyo lakini Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi, na muda sio mrefu tutakamilisha.” amesema Kamanda Sabas.

 

“Kuhusu baadhi ya video kusema kwamba huyu Mtu ni Mkazi wa Upanga sisi hatuthibitishi mambo kupitia clips za video, tunathibitisha mambo kupitia upelelezi kwahiyo upelelezi ndio utakaoeleza, kuhusu swali la Waandishi kuhusu kuwepo kwa dalili zozote za ugaidi kwenye tukio la leo hatuwezi kusema chochote hii ni mapema lakini uchunguzi ndio utakaosema kama kuna ugaidi au hakuna ugaidi.

 

“Kwa sasa hatuwezi kusema amekutwa na kitu gani mfukoni, Polisi bado wapo eneo la tukio… ni mapema sana kusema amekutwa na nini kwasababu Wataalamu wapo kazini, kuhusu kama ni Raia kama sio Raia uchunguzi ndio utasema baada ya upelelezi kukamilika tunachojua sasa huyu ni Muhalifu,” amesema  Kamishna Sabas.

 

Kamishna Sabas ameongeza kuwa watu sita wamejeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wanakoendelea kupatiwa matibabu, na kueleza kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi na utakapokamilika, taarifa itatolewa.

 

Leave a Comment