
MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania, (IGP) Simon Sirro amethibitisha kuuawa kwa askari wawili wa Jeshi la Polisi wakati wa mapambano ya kurushiana risasi yaliyotokea katika maeneo ya daraja la Salenda karibu na Ubalozi wa Ufaransa, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo la aina lililozua taharuki miongoni mwa wananchi limetokea leo Jumatano, Agosti 25, 2021 baada ya mtu mmoja mwenye asili ya Somalia ambaye hajafahamika kuzua taharuki baada ya kufyatua hewani risasi huku akisikika akisema kuwa anawatafuta polisi.
Akizungumza katika kikao kazi cha maofisa wa polisi kinachoendelea katika Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar, Sirro amethibitisha kuwa mtu huyo naye ameuawa kwa kupigwa risasi.
“Nimeona clip zinaruka sasa hivi, mtu huyo aliingia barabarani akawa anatamba na SMG, akapigwa risasi na polisi, kwa hiyo ameua askari wetu wawili nayeye ameuawa. Majeshi yetu yapo eneo la tukio, tutajua ametoka wapi, ni nani na baadaye nitawapa taarifa. Hiyo ndio kazi yetu, awiii….! waaaa…..! awiiii…..! waaaaa!,” amesema IGP Sirro.
Ameeleza kuwa wanaendelea kufuatilia kufahamu mtu huyo ametokea wapi na baadaye watatoa taarifa kamili.