×

Kivuko cha MV. Tegemeo Charejea, Chaanza Kupiga Kazi Buchosa – Video

HATIMAYE huduma za Kivuko cha MV. Tegemeo kinachofanya safari zake Kati ya Kijijicha cha Kahunda (Halmashauri ya Buchosa) – Sengerema, Kisiwa cha Maisome (Wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza) na Kijiji cha Nkome (Wilayani Geita Mkoa wa Geita) zimerejea upya baada ya kivuko hicho kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Mapokezi hayo yamenafanyika Agost 29, 2021 katika Kijiji cha Busikimbi, Kisiwa cha Maisome yakiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga na mbunge wa Jimbo la Buchosa, Mhe. Eric Shigongo na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi wa eneo hilo pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Diwani wa Kata ya Maisome Dauson Miyaga.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, DC Ngaga amesema watendaji wa Serikali waofanya kazi kwenye kivuko hiki amewataka wakitunze na kidumu ili kiendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.

 

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo Buchosa, Eric Shigongo amesema ukarabati wa Kivuko hicho ni niutekelezaji wa Ilani ya CCM na moja ya ahadi zake juu ya kukarabati kwa kivuko hicho ili kiendelee kuwahudumia wananchi.

Shigongo amesema baada ya kukamilisha Kivuko hicho na kurejesha  safari zake kama awali, mwezi Oktoba, mwaka huu Serikali itakabidhi kivuko kingine kipya katika Kisiwa cha Kome ili kuwaondolea adha wananchi wa maeneo hayo na kurahisisha usafirishaji wa mazao yao ya chakula pamoja na samaki na mengine.

“Tuendelee kumuunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan, anayo nia njema ya kuiletea maendeleo thabiti Buchosa yetu, mniunge mkono mimi mbunge wenu pamoja na diwani wenu, tukiunganisha nguvu, Buchosa ndani ya mda mfupi itabadilika na wananchi watapata maendeleo,” amesema Shigongo.

Mmoja wa Wananchi wa kisiwa cha Maisome Baraka Bituro amesema kurejea kwa huduma ya usafiri kwenye Kisiwa hicho imekuwa mkombozi kwao. Wananchi wa Kisiwa cha Misome wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kukifanyia ukarabati Kivuko  hicho na sasa biashara zao na shughuli zao za kiuchumi zitakimbia haraka kwani zilikuwa zikikwamishwa na miundombinu ya usafiri.

Meneja wa Tamesa Mkoa wa Mwanza Hasan Karonda amesema ukarabati huo umegharimu kiasi cha Tsh milioni 672 na umedumu kwa miezi sita mpaka kukamilisha ukarabati huo. Koronda amesema ukarabati huo ni pamoja na kufunga injini mbili mpya na kisasa ambapo kimepewa jina la MV Tegemeo Kazi Inaendelee.

Awali, Kivuko cha MV Tegemeo kilizinduliwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wakati huo) Dkt. Mohamerd Bilal mnamo Sepetemba 26/2014 katika Kijiji cha Kahunda Wilayani Sengerema.

Amesema Kivuko cha MV Tegemeo chenye uzito wa tani 85 kina uwezo wa kubeba magari 10, abiria wapatao 200 na mizigo kwa wakati mmoja, wakati kikifanyiwa ukarabati, Kivuko cha MV Chato kilikuwa kikisaidia kutoa huduma kwa wananchi wa Kisiwa cha Maisome na Kahunda hadi Nkome.

“MV Tegemeo ilisitisha kutoa huduma zake kati ya Kisiwa cha Maisome na Nkome Geita mwezi Januari, mwaka huu baada ya injini zake kuharibika na ukarabati huu umekamilika kwa kipindi cha miezi sita. Ukarabati huu utadumu kwa miaka sita ijayo bila kufanyiwa matengenezo makubwa,” amesema Karonda.

 

 

Serikali ya awamu ya nne ilitengeneza kivuko hicho kufuatia baadhi ya wakazi wa Kisiwa cha Maisome kupoteza maisha mara kwa mara wakati wakivuka kwenda Kijiji cha Kahunda na Nkome Geita kutafuta mahitaji wakitumia mitumbwi ya kupiga kasia na mitumbwi ya kutumia injini.

Leave a Comment