
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imetoa azimio mbunge wa Ukonga Jerry Silaa asimamishwe kuhudhuria mikutano miwili ya bunge mfululizo na aondolewe kwenye nafasi ya uwakilishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika (PAP).
”Kamati ilimhoji Mh. Jerry Silaa ili kuthibitisha kauli yake kuwa mishahara ya wabunge haikatwi kodi na aliuzwa iwapo mshahara wake unakatwa kodi au haukatwi alisema kuna sehemu inakatwa kodi na kuna sehemu haikatwi kodi.
”Katika mahojiano Mh. Jerry Silaa alikiri kuwa kauli zake zimeleta tafrani kwenye jamii, uchambuzi wa ushahidi wa sheria kwenye shauri hili unathibitisha kuwa alikuwa na nia ovu ya kulidharau na kulidhalilisha bunge pamoja kuchonganisha bunge, serikali, uongozi wa bunge na wananchi,” ameserma Emmanuel Mwakasaka, mwenyekiti wa Kamati ya Maadili.
Kilichomponza Silaa ni kauli yake kuwa wabunge hawalipi kodi katika mishahara yao jambo lililoelezwa ni uongo kwani wabunge wanalipa kodi.