
WAZIRI wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Rais Samia Suluhu Hassan amepunguza tozo za miamala ya simu ili zisiwaathiri vijana wengi waliojiajiri kwenye huduma za fedha kwa njia ya simu. Amewataka Watanzania kutochukulia tozo kama uhasama, bali njia ya kuboresha maisha yao.
Mwigulu amesema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari jijini Dodoma na kuongeza kuwa, Rais Samia ameelekeza fedha zote zitakazokusanywa kwenye tozo za miamala ya simu kuanzia leo Septemba Mosi zielekezwe kwenye sekta ya elimu (kujenga/kukarabati madarasa na madawati) ili kupanua fursa ya elimu kwa watoto wengi zaidi.
Dkt. Mwigulu pia amesema idadi ya miamala ya simu kabla ya tozo na baada ya tozo inalingana, ambayo ni kati ya miamala 10 hadi milioni 11. Amekanusha madai kuwa tozo za miamala zimeshababisha kupungua kwa miamala ya fedha kwa njia ya simu.
“Mheshimiwa Rais ameelekeza uangaliwe mfumo mzima wa mapato na matumizi, maeneo ambayo yana mianya ya upotevu wa fedha hivyo tunawahakikishia Watanzania kwamba mambo hayo yanaangaliwa.
“Kabla ya kuanza kwa tozo kulikuwa na miamala milioni 10 hadi milioni 11 lakini sasa kuna miamala milioni 10, milioni 9.8, milioni 9.9, hata juzi Agosti 24, 25, 28, 29 miamala ilikuwa ni milioni 10 kama ilivyokuwa kabla ya kuanza utekelezaji wa tozo
“Tangu tuanze hilo zoezi [kukusanya tozo za miamala] mpaka tarehe 30 [Agosti] tuna zaidi ya bilioni 63. Fedha zote zitakazokusanywa kwenye tozo za miamala ya simu kuanzia leo Septemba 1, zitajenga vituo vya afya 220 kwenye tarafa zote nchini ambazo hazikuwahi kuwa na vituo vya afya tangu uhuru. Vituo hivyo vitakuwa na maabara na kutoa huduma za upasuaji.
Aidha, Mwigulu amewaonya wafanyabiashara wanaowafundisha Watanzania kukwepa kodi kwa kuwapa bei mbili za bidhaa, bei yenye risiti na bei isiyo na risiti. Amesema kuna wafanyabiashara wakidaiwa risiti wanajivuta, mara wanafuta mashine vumbi, hadi anayedai risiti akate tamaa.
“Wamiliki wa nyumba wasihamishie huo mzigo [kodi ya majengo] kwa wapangaji. Mmiliki atakayefanya kiburi na kutaka kuhamishia kwa wapangaji, atakuwa anakiuka sheria. Atakayefanyiwa hivi, aje anione hata mimi ofisini.”- Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba.
“Tumetengeneza timu ya wataalamu ya kuangalia mfumo mzima wa masuala ya kodi na matumizi lengo likiwa ni kuangalia kwanini kwenye masuala ya makusanyo inaleta maumivu, tumekuja kugundua kuna mahali hatuko sawa kwenye mfumo wa makusanyo.
“Mimi ninayefanya kazi ya usaidizi kwenye upande wa fedha karibu na raisi niwahakikishie, rais wetu ana dira nzuri sana kwenye masuala ya maendeleo lakini pia analiona kwa ukaribu sana jambo hili linalohusu mfumo wa makusanyo na matumizi,” amesema Dk. Mwigulu Nchemba.