
MWILI wa marehemu mzee Wilson Ogeta Owit ( 89) mkazi wa Kijiji cha Nyambogo wilayani Rorya mkoani Mara umeshindikana kuzikwa kwa miezi 8 kwa kusalia katika chumba cha kuhifadhia maiti Utegi kutokana na mgogoro wa ardhi baina ya wanafamilia na mtu aliyenunua eneo lao.

Katika sakata hilo, familia ya marehemu iligoma kuzika wakidai kuwa eneo ambalo limetengwa na familia kwa ajili ya maziko ya mzee huyo na wanafamilia wengine limeng’ang’aniwa na mtu mmoja anayedai kuwa alilinunua kwa marehemu jambo ambalo familia iligoma.

Lakini baada ya familia na mtu aliyenunua ardhi ya marehemu kukutanishwa na familia ya marehemu, wanafamilia hao imekubali kuzika sehemu nyingine kisha kuangalia namna ya kutatua jambo hilo kisheria.

Mzee Owit amezikwa jana Alhamisi, Septemba 3, 2021 kwa usimamizi wa Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka ambaye alizikutanisha pande zote mbili zilizokuwa na mgogoro huku wanafamilia wa marehemu wakiiomba serikali kusimamia eneo la marehemu kurejeshwa kwa mjane ili kuendeleza shughuli za uzalishaji.

“Niwaombe ndugu zangu tuwe na subira katika kipindi hiki serikali ikifatilia kwa ukaribu jambo hili, nimeletwa hapa kutatua kero za wananchi niwaombe sana hakuna kitakachoharibika na kazi ya serikali ni kutetea wanyonge,” Juma Chikoka, DC Rorya.
