
ALIYEKUWA Rais wa Afghanistan kabla ya Taliban kuichukua, Ashraf Ghani, amewaomba msamaha watu wa nchi hiyo baada ya kukimbilia nchi za Falme za Kiarabu na kusema aliondoka baada ya kushawishiwa na usalama wa Ikulu kwamba angeendelea kuwepo kungehatarisha maisha ya raia.
Ghani aliondoka ghafla nchini Afghanistan wakati wanamgambo wa Taliban walipokuwa wakiendelea kuingia kwenye mji mkuu mnamo Agosti 15. Alisema hakuwa na nia ya kuwaacha watu wake lakini “ilikuwa ndio njia pekee iliyosalia.”
Katika taarifa iliyoshirikishwa kwenye mtandao wa Twitter siku ya Jumatano, Bw. Ghani alisema hakuwa na njia nyingine yoyote zaidi ya kuondoka nchini humo ili kuepusha kuenea kwa ghasia.
“Kuondoka Kabul ulikuwa uamuzi mgumu zaidi maishani mwangu,” amesema, akiongeza kuwa anajuta kwamba “hakuweza kumaliza hilo kwa njia tofauti.”
“Niliondoka kwa kushawishiwa na usalama wa ikulu, ulionishauri kuwa kuendelea kuwepo kulihatarisha kutokea kwa mapigano mitaani na katika barabara za mji kama ilivyotokea wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka ya 1990,” aliandika, akiongeza kuwa alifanya hivyo kuokoa mji wa Kabul na raia wake milioni sita.
Alisema alikuwa amejitolea kwa kipindi cha miaka 20 kusaidia Afghanistan kuwa nchi ya kidemokrasia, mafanikio na huru. Ghani ameongeza kuwa alikuwa na “masikitiko makubwa” kwamba “muda wangu mwenyewe uliishia kwa majuto kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wangu.”