
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema ameamua kuvunja mwiko wa kwamba Wizara ya Ulinzi lazima akae mwanaume mwenye misuli yake, la hasha, hata mwanamke anaweza kuiongoza vizuri wizara hiyo kwa kufanya yale yanayotakiwa.
Rais Samia amesema hayo leo Jumatatu, Septemba 13, 2021 wakati akizungumza kwenye hotuba yake ya kuwaapisha mawaziri aliyowateua jana na kuongeza kuwa kazi ya Waziri sio kupiga mizinga wala kubeba mabunduki, ni kusimamia sera na utawala wa Wizara. Nikaamua dada yetu Dkt. Stergomena Tax nimepeleke huko.
“Dkt. Stergomena nimempeleka huko si tu kwa kuvunja huo mwiko, ni sababu ya upeo wake mkubwa alioupata akiwa SADC. Kwa uzoefu wake hasa kwenye sekta ya ulinzi atatusaidia. Anawajua askari wetu walioko Msumbiji, DRC, mifumo yao, haki zao, atamsaidia vizuri CDF.
“Makamba sio mgeni nenda kafanye kazi. Mbarawa hii sekta unaijua vizuri (Wizara ya Ujenzi). Hivyo ni matumaini yangu mtakwenda kufanya vizuri, uteuzi wenu sio kwamba nyie ni wazuri sana kuliko wengine waliokuweko, uzuri wenu utatokana na utekelezaji wa majukumu yenu.
“Nimeamua kufanya mabadiliko ya watu watakaoongoza hizo Wizara. Ulinzi ni Dkt. Stergomena, Habari ni Ashatu ambayo ni Wizara nzito sana japo utekelezaji wake ulikuwa unachukuliwa kwa wepesi, nenda kafanye kazi.
“Ninachotaka kuona ni matokeo, sio kuwaona tu kwenye TV, tupo hapa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi. Muende mkaanze kwa kasi, pale ambapo wenzenu walipoachia, mkikuta kuna sehemu ya kufanya mabadiliko fanyeni, muende kwa haraka sana, muda hautusubiri.
“Mabadiliko sio kwa nyie wageni tu hata kwa mawaziri wa zamani, nendeni mkajipange upya, tuone tunatoa huduma gani kwa wananchi,” amesema Rais Samia.