×

Tanzia: Profesa Luhanga Afariki Dunia

ALIYEKUWA Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Matthew Luhanga (73) amefariki dunia jana Alhamisi, Septemba 16, 2021, jijini Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu.

 

Mratibu wa Mawasiliano na Habari wa UDSM, Dkt. Dotto Kuhenga amesema; “Ni kweli tumempoteza Profesa Luhanga ambaye alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo chetu kwa muda mrefu. Siwezi kuzungumzia zaidi kuhusu ugonjwa wake lakini alikuwa amelazwa hospitali,” amesema Dk Kuhenga.

 

Dkt. Kuhenga ameeleza wasifu wa Profesa Luhanga akisema aliajiriwa rasmi katika chuo hicho kama mhadhiri mwaka 1978 baada ya kufanya kazi hiyo kwa miaka miwili kama mhadhiri wa muda wakati huo akiwa ofisa elimu.

 

Amesema mwaka 1982, alipandishwa cheo na kuwa mhadhiri mwandamizi. Mwaka 1986, alipanda na kuwa profesa mshiriki na mwaka 1990 akawa profesa kamili, akiwa ni mmoja kati ya maprofesa wachache nchini waliofikia hatua hiyo.

 

“Mbali na kuwa kiongozi wa chuo, Profesa Luhanga amekuwa mjumbe wa bodi mbalimbali na ameandika machapisho mengi hasa katika sekta aliyobobea ya telecommunication (mawasiliano),” amesema.

 

Elimu

Kuhusu elimu yake, Dk Kuhenga amesema mwanazuoni huyo alisoma shahada yake ya awali katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha California kati ya mwaka 1970 – 1974 ambapo alisomea masuala ya uhandisi wa umeme (Electrical and Electronic Engineering).

 

Vilevile, alisomea shahada ya uzamili ya mawasiliano ya kompyuta katika Chuo Kikuu cha Columbia mwaka 1984 na katika chuo hicho hicho, alifanikiwa kutunukiwa shahada ya uzamivu katika mawasiliano ya komputa.

 

“Profesa Luhanga alikuwa full professor ndani ya muda mfupi tangu alipokuwa associate professor, hao watu wako wachache hapa nchini, wengi tulionao ni associate professors,” amesema Dk Kuhenga.

Leave a Comment