
MABINGWA wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga Jumapili hii wanatarajia kuwa katika viunga vya Port Harcout nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao Rivers United.
Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kipigo cha bao 1-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza, ambao ulipigwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga ilikumbana na kipigo hicho ikiwa imepita wiki moja tu, tangu wapoteze kwa mabao 2-1 dhidi ya Zanaco FC kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki katika siku ya kilele cha Wiki ya Mwananchi ambayo ilifanyika kwenye huohuo.
Kutokana na matokeo hayo ya mchezo wa kwanza, Yanga sasa wana kibarua kigumu cha kuhakikisha wanapindua meza ugenini kwa kuhakikisha wanaibuka na ushindi tofauti ya kuanzia mabao 2-0, au zaidi ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya kwanza ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Barani Afrika.
Kwangu hili naamini linawezekana licha ya kwamba wengi wanaona linaweza kuwa jambo gumu kutokana na changamoto ya kuchezea katika ardhi ya ugenini, lakini binafsi naamini kuwa bado Yanga wana nafasi kubwa kupata matokeo mazuri.
Ni kweli Rivers wametangulia baada ya kupata ushindi hapa Tanzania, lakini hiyo haitoshi kuwa sababu ya kushindwa kupata matokeo kwenye mchezo wa marudiano, hivyo Yanga wana nafasi nyingine ya kufanya maajabu huko Nigeria.
Ni muda sasa kwa benchi la ufundi chini ya kocha mkuu, NassredineNabi kufanyia maboresho mapungufu yaliyojitokeza kwenye dakika tisini za Dar es Salaam, ili yasiweze kujirudia kwenye mchezo wa marudiano.
Kiufundi Yanga walizidiwa kwenye maeneo mengi, hawakuwa na nidhamu ya ukabaji, wala umakini katika safu ya ushambuliaji, jambo ambalo liliwapa uhuru wachezaji wa Rivers kuutawala mchezo vile wanavyotaka.
Timu haikuwa na muunganiko mzuri kuanzia eneo la ulinzi, kiungo na eneo la ushambuliaji, pia uzito kwenye kufanya maamuzi ya haraka kwa mchezaji mmoja mmoja lilikuwa ni tatizo lingine ambalo Yanga walikumbana nalo kwenye mchezo huo.
Msimu huu Tanzania imeingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa, hivyo ni wajibu kwa timu zote ambazo zinashiriki michuano hii kupambana vilivyo ili tuweze kuzilinda nafasi hizi msimu ujao. Hili litawezekana pale tu timu zitakapopambana kupata matokeo katika kila mchezo ambao wanashuka dimbani.
Wachezaji wanapaswa kutambua kuwa wamebeba jukumu zito la kuipambania nembo ya Yanga na taifa kwa ujumla, kwani timu inavyozidi kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa inazidi kuipandisha thamani ligi yetu ambayo kwa miaka ya hivi karibuni inazidi kukua.
Mashabiki pia hiki ndiyo kipindi ambacho mnapaswa kuwa karibu na wachezaji kwa kuwapa sapoti kwenye kila hatua wanayopitia, na si kutumia muda mwingi kukosoa. Watanzania tunaamini katika jeshi la Yanga huko Nigeria kwani kiuhalisia mwanajeshi wa kweli hachagui uwanja wa vita.