
UKIACHANA na utajiri wake wa mashairi makali na mpangilio mzuri wa sauti, staa mwingine wa Bongo Fleva, Raymond Shaban Mwakyusa au Rayvanny ameonesha utajiri mwingine wa mali na pesa kiasi cha kumshtua bosi wake, Nasibu Abdul almaarufu Diamond Platnumz, IJUMAA lina ripoti kamili.
Kwa mambo makubwa aliyoyafanya bwa’mdogo huyo aliye chini ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), ni dhahiri kutamka kwamba, ana hasira ya kusaka mafanikio na muziki unalipa endapo mtu ataufanya kwa bidii kubwa na malengo!
Rayvanny ambaye historia yake ya muziki ilianzia Tip Top Connection chini ya Mkubwa Fela kabla ya kujiunga WCB mwaka 2016, amefanikiwa kumiliki mali mbalimbali ambapo kwa jumla inatosha kumuita bosi.
MALI ZENYEWE
Ndani ya wiki chache, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, Rayvanny amefungua mgahawa wake wa kifahari uliopo maeneo ya Massana, Mbezi-Beach jijini Dar.
Staa huyo amefanikiwa kufungua mgahawa huo ambao Gazeti la IJUMAA limeushuhudia ukiwa ni wa hadhi kubwa mno ambapo amewakaribisha wadau, hasa mastaa wenzake kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
MJENGO WA KISTAA
Ni katika kipindi hichohicho ambacho Rayvanny au Vanny Boy ameonesha mjengo wa kistaa anaojenga maeneo ya Tabata- Kifuru jijini Dar ambao ndani yake una kila kitu kinachostahili kuwepo kwenye nyumba za mastaa kama maegesho makubwa, bwawa la kuogelea, vyumba vya kutosha vya kulala na kupumzika.
Zipo taarifa pia kwamba yupo mbioni kukamilisha ujenzi wa klabu ya starehe nyumbani kwao huko jijini Mbeya ambayo itakamilika muda si mrefu.
LEBO YA NEXT LEVEL MUSIC
Ukiacha mgahawa, nyumba anayojenga na klabu ya usiku, mapema mwaka huu, Rayvanny alizindua lebo yake ya muziki iitwayo Next Level Music (NLM) yenye ofisi zake za maana na kueleweka zilizopo Mbezi-Salasala jijini Dar.
Hata hivyo, pamoja na kumiliki lebo yake hiyo, lakini bado anaendelea kuwa chini ya WCB ya mtu mzima, Diamond.
MAUZO YA KUTISHA
Ripoti ya mauzo (streams) kwenye mitandao ya kusikiliza, kutazama, kununua na kuuza muziki kama Spotify, Boomplay, Tidal, Itunes, YouTube, Audiomack, Apple Music na mingine mingi, jamaa huyo anatisha kwa kushika nafasi ya pili kwa mwaka huu wa 2021 akiwa ametanguliwa na Diamond Platnumz pekee.
Kwa mujibu wa mtu wake wa karibu, Baba Levo, mavuno ya Rayvanny ya ghafla kwa mwaka huu kwenye mitandao hiyo ni makubwa kiasi kwamba hata Diamond au Mondi mwenyewe ametishika na kuona kama dogo anataka kumpiga kikumbo.
“Rayvanny ndiye msanii wa pili kwa mauzo ya muziki kwenye mitandao kwa Tanzania, mimi mwenyewe natamani kufanya naye nyimbo hata 130,” anasema Baba Levo.
Pamoja na kwamba kwa sasa anaishi kwenye nyumba ya kupanga, lakini muda siyo mrefu atahamia kwenye mjengo huo wa ghorofa anaojenga.
NDINGA KALI
Kuhusu usafiri, Rayvanny au Chui anamiliki magari madogomadogo, lakini pia ana ndinga aina ya Toyota Land Cruiser Prado la rangi nyeusi amblo ni gari kali la ndoto yake.
Uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA umejiridhisha kwamba, siyo wengi wanajua kiwango cha utajiri wa Rayvanny ilikilinganishwa na wasanii Kama Diamond na Harmonize.
Kuna maelezo mengi kwenye mitandao kuhusiana na utajiri wa Diamond au Harmonize, ila kwa utajiri wa Rayvanny, ni mitandao michache mno yenye data kama hizo zinazopatikana ndani ya Gazeti la IJUMAA pekee.
Rayvanny mwenye umri wa miaka 28 na mzaliwa wa jijini Mbeya, anatajwa kwenye orodha ya wasanii matajiri Bongo. Ni msanii aliyepitia maisha magumu kabla hajakutana na Diamond Platnumz. Kusema kweli, Diamond amechangia pakubwa kwenye mafanikio yake.
UTAJIRI BIL. 2.3
Utajiri wa Rayvanny unakadiriwa kufikia Dola za Kimarekani milioni moja (zaidi ya shilingi bilioni 2.3 za Kitanzania) ambazo ni jumla ya mali zote, mauzo ya muziki wake na shoo mbalimbali anazofanya ambazo siyo chini ya shilingi milioni 50 kwa shoo moja.
ALIKOTOKA RAYVANNY
Rayvanny alianza kujulikana mwaka wa 2016 alipoachia Wimbo wa Kwetu chini ya WCB, lakini kabla ya hapo alikuwa ‘amehaso’ ile mbaya.
Nyimbo zingine za Rayvanny zilizofanya vizuri ni pamoja na Chuchuma, Tetema, Pepeta, Vumbi, Amaboko, Zilipendwa, Zezeta, Lala na nyinginezo kibao, lakini kubwa zaidi ni mafanikio makubwa aliyoyapata kupitia albam yake ya Sound From Africa na EP mbili za Flowers na Vanny Boy.
STORI: MEMORISE RICHARD, DAR