
WASTARA Juma si jina geni kwenye Bongo Movies. Ni mwanamama aliyefanya na anafanya vizuri kwenye filamu nchini Tanzania na wenye ushawishi mkubwa.
Wastara amezaliwa Septemba 27, 1983 mkoani Morogoro. Mwaka 1989 alijiunga na Shule ya Msingi Mvomero A na kufanikiwa kumaliza elimu yake ya msingi mwaka 1995. Mwaka 1996, alijiunga na Sekondari ya Agricalture mkoani humo.
Mwaka 1999, Wastara aliingia rasmi kwenye sanaa ya maigizo na filamu yake ya kwanza kucheza iliitwa Utaishia kunawa akiwa na aliyekuwa gwiji wa vichekesho Bongo, marehemu King Majuto.
Mwaka 2004 hadi 2006, Wastara alianza kuonekana kwenye mchezo wa Miale uliokuwa unarushwa na Television ya ITV.
Wastara hakudumu kwenye mchezo huo, alikutana na kina Jenifa Mgendi ambaye pia walifanikiwa kuigiza naye filamu iliyowashirikisha baadhi ya wasanii wa kitambo akiwamo Dino na wengineo.
Mwaka 2007, Wastara alifanya usahili kwenye filamu ya Ande John iliyofahamika kama Peremende, akafaulu na kuigiza kwenye filamu hiyo kisha zikafuata filamu nyingine kama Penina kabla ya kutimkia nchini Kongo kufanya biashara.
Aliporejea kutoka Kongo, Julai, 2007, Wastara aliitwa na mwigizaji Shija ambaye alimuomba aigize naye filamu baada ya kumuona kupitia kazi mbalimbali alizowahi kufanya.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa Wastara kukutana na Sajuki ambaye alimuoa na kujaaliwa kupata naye mtoto mmoja kabla ya kufikwa na umauti tarehe 2 mwezi wa kwanza mwaka 2013, lakini hadi sasa anaendelea kufanya vizuri kunako Bongo Movies.
Licha ya kujikita zaidi kwenye filamu, mwanamama huyo amekuwa akijishughulisha na kazi mbalimbali, yaani ni mjasiriamali; ni muuzaji wa nguo na vipodozi vya wanawake akiwa ni mama wa watoto watatu.
Hata hivyo, baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu, Wastara amekuwa akipokea maswali mengi kutoka kwa mashabiki wake wakitaka kujua kwa nini yupo kimya.
Kupitia gazeti namba moja la mastaa ndani na nje ya Bongo la IJUMAA, Wastara ameamua kuwajibu mashabiki wake huku akieleza namna alivyougua kwa muda mrefu na kudhoofika mwili;
IJUMAA: Kwa nini umepotea kwenye uingizaji wa filamu?
WASTARA: Kiukweli sijapotea ila ni kwa sababu ya changamoto mbalimbali zinazonisababisha niwe kimya.
SWALI: Ni changamoto gani zilizokusababisha uwe kimya kwa kipindi kirefu?
WASTARA: Nimeugua kwa muda mrefu ambapo nilidhoofika kimwili na pia kuna kushuka kwa tasnia ya filamu.
SWALI: Kwa huo muda ambao ulikuwa kimya kwenye filamu ulikuwa unajishughulisha na vitu gani?
WASTARA: Nilikuwa najishughulisha na biashara.
SWALI: Kuna biashara za aina nyingi, wewe ulikuwa umejikita kwenye biashara gani?
WASTARA: Nilikuwa najishughulisha na uuzaji wa nguo na vipodozi ambapo kidogo nilichokuwa nakipata ndiyo nilikuwa najikimu kwenye matumizi madogomadogo.
SWALI: Tumeona unafanya filamu na biashara, katika vitu hivyo viwili ni kipi ambacho kilikuwa kinakulipa kuliko kingine?
WASTARA: Siwezi kusema ni kipi kimenilipa zaidi ya kingine, lakini kiukweli kwenye Bongo Movies tunafanya kazi kwa pesa kubwa, lakini tunakwenda kuiuza kwa pesa ndogo, hiyo inatufanya tushindwe kuigawa pesa kwa sababu waigizaji wa filamu moja ni zaidi ya watu 10 hivyo wanaofaidika ni wanaouza filamu na siyo waigizaji.
SWALI: Kwa kusema hivyo, unamaanisha kuwa Bongo Movies hazikulipi ukilinganisha na biashara?
WASTARA: Ha ha ha hapana…
SWALI: Umepanga kurudi na gia gani ili kuwarudisha mashabiki wako?
WASTARA: Siyo kwamba nitarudi kwa kasi ya 4G au kwa mikiki ila nitakuja kwa kuonesha uwezo mkubwa katika kazi na mashabiki wataniona na kuzipenda na kuzidi kuzifuatilia kazi zangu hivyo nataka kuwaambia kuwa wasijali.
SWALI; Unawaambiaje wadau wako?
WASTARA; Nawaambia wakae mkao wa kula kwa kuzipokea kazi zangu ambazo zitatoka mwisho wa mwaka huu.
Stori; Penina Mchomvu na Neema Shaweji, Bongo