×

Rais Samia Atoa Maagizo Mazito ALAT – Video

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameshiriki mkutano mkuu maalum wa uchaguzi wa viongozi wa jumuiya ya tawala za mitaa tanzania – ALAT katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center jijini Dodoma, Leo 27 septemba, 2021.

 

“Mkutano huu ni wa kwanza tangu tumalize uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, kwa hiyo ninawapongeza sana madiwani, mameya kwa kuchaguliwa, pia wakurugenzi kwa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Mkutano huu.

 

“Uchaguzi wowote hauna dogo, hata uchaguzi wa Mkuu wa darasa “monitor” una mambo yake, najua wapiga kura hapa wanasubiri karatasi zisogezwe wafanye yao, wagombea nao matumbo joto.

 

“Mtakaochaguliwa mkaendeleze majukumu ya ALAT kama ilivyosajiriwa kisheria, kubadilishana mawazo na kuwa na mijadala na utetezi wa sera na sheria zinazohusu serikali za mitaa, mkayapigie debe, kama kuna tatizo mtuandikie mlete Serikalini tutalifanyia kazi.

 

“Kazi ya pili ya ALAT ni kusambaza habari na kutoa elimu kwa Serikali za Mitaa, na tungependa ALAT ichemke katika hilo. Kuwa na uwakilishi na kupeleka mapendekezo Serikalini na Jumuiya za Kimataifa.

 

“Maagizo yangu kwa ALAT ni kutumia mitandao katika kazi zenu, kutoa taarifa za Serikali za Mitaa, kukusanya mapato, kuweka rekodi za huduma zinazotolewa kwa wananchi.”

 

“Pamoja kwamba tutaleta fedha na tutaendelea kuleta, lakini thamani ya fedha kwa miradi inayotekelezwa ionekane, huo ndio wajibu wenu na liwe la kwanza katika utekelezaji wenu. Kuna migogoro mikubwa ya ardhi kwa sababu taarifa haziko sawa.

“ALAT mkasimamie makusanyo na matumizi ya fedha, Serikali inaleta fedha lakini kinachotoka kwenu ni kidogo sana, yawezekana hakikusanywi ama kikikusanywa kinaishia kwenye mifuko ya watu na si kwa wananchi.

 

“Tanzania tulichagua kutokuwa na njaa, kuondoa umasikini, huduma safi za afya, elimu, maji, kujenga miundombinu, kukuza uchumi na kukuza mabadiliko ya tabia ya nchi, uongozi utakaochaguliwa mkayasimamie haya.

 

“Mfuko huu ulikuwa unatumika kama mfuko wa kisiasa wa madiwani, kila diwani anapeleka kwake vijipesa kujipendekeza kwa watu ili ateuliwe, lakini huoni marejesho wala kilichofanyika, sasa mjipange kutoa fedha kwa vikundi vikubwa vyenye miradi mikubwa itakayoleta tija.

 

“Mnatoa Tsh milioni 40 kwa kikundi au Tsh mil 100 lakini mnajua watakwenda kufanya mradi mkubwa, wataajiri wenzao na faida itaonekana sio kutoa fedha kidogo kidogo kujipendekeza kwa wapiga kura ili uje kuteuliwa, mfuko huu tunauua.”Ubadhirifu wa fedha ukawe histioria huko tunakokwenda.

 

“Fedha zinaletwa kwenu lakini thamani ya miradi haiendani. Juzi nilimuona Waziri Mkuu ameenda sehemu kuzindua (TANESCO Kyerwa), kibanda kinasemwa kimejengwa kwa milioni kadhaa, kimepakwa rangi tu mbele, mamilioni yamemiminika pale, nataka thamani ya fedha ionekane.

 

Tutaendelea kupeleka fedha kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuendelea kutekeleza miradi ambayo itaboresha huduma kwa wananchi wetu,” amesema Rais Samia.

 

Leave a Comment