
KWA mara nyingine NHC imeaminiwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kupewa dhamana ya kuwa Mkandarasi wa jengo la Makao Makuu ya Ofisi za Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari litakalochukua miezi 24 hadi kukamilika kujengwa eneo la Mtumba Jijini Dodoma, Jengo hilo litakalogharimu shilingi bilioni 23.948 ni la sita kupewa NHC hadi sasa.
Miradi ya Wizara zingine ambazo Shirika imeshapata na fedha zake zikiwa kwenye mabano ni Sanaa, Utamaduni na Michezo (22.843 bilioni), Wizara ya Madini (22.848 bilioni), Wizara ya Mifugo na Uvuvi (23.239 bilioni), Wizara ya Biashara na Viwanda (22.9 bilioni) na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (22.350 bilioni).
Akitoa maelezo ya Serikali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa Serikali ina imani kubwa na NHC kutokana na kazi nzuri inazofanya na akasisitiza kuwa Wizara hiyo inatarajia kupata jengo lenye ubora mkubwa. Amesema kuwa Serikali inakusudia kuufanya mji huo kuwa wa kijani kwa kupanda miti na kuwa na matumizi ya nishati inayokubalika duniani.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika eneo la ujenzi wa Jengo la Wizara hiyo, mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa NHC Dkt Maulidi Banyani aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuliamini Shirika la Nyumba la Taifa na akaihakikishia Serikali kuwa NHC itatekeleza miradi iliyopewa kwa weledi, ubora wa hali ya juu, katika muda uliowekwa au chini ya muda na gharama zilizokubalika.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa ana imani na NHC na Mshauri Mwelekezi, TBA kwa kuwa wana uzoefu mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba. Ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa ili kuwezesha ujenzi wa jengo hilo kukamilika kwa wakati.
Wakati huo huo, Katibu wa Kikosi Kazi cha Utekelezaji wa Mji wa Serikali na Kuhamia Dodoma Bw. Meshack Bandawe amesema kuwa Serikali imetumia shilingi bilioni 163 kuhamishia Dodoma jumla ya watumishi 18,000 wa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali na kwamba Mji wa Serikali unaendelea kuwekewa miundombinu ya kisasa barabara, maji, umeme wa chini, mifumo ya Tehama na usafiri wa treni utakaosaidia Wananchi kupata huduma katika mji huo wa Serikali.
Akabainisha kuwa mji huo wa Serikali umejengwa katika utaratibu wa kuzingatia kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali na utakuwa na hadhi ya Mji wa Kijani(greencity).