
UKITAJA namba za wasanii wanaofanya poa kwa sasa kweye kiwanda cha muziki mtamu wa Bongo Fleva na Amapiano, huwezi kuacha kutaja jina la mwamba Omary Mwanga ila kwa wapenzi wa kazi zake wanamtambua kwa jina la Marioo au Toto Badi.
Kijana huyu alianza kuwika miaka michache iliyopita. Alijulikana na ngoma yake inayokwenda kwa jina la Dar Kugumu uliorekodiwa mwaka 2017 ambapo ulitisha kiasi cha kushika nambari moja kwenye platforms mbalimbali za muziki duniani.
Mbali ni uimbaji wake, Marioo pia ni mtayarishaji mmoja mzuri wa ngoma za wasanii wenzake. Amemtungia ngoma bomba kabisa mwanadada anayesumbua kwa sasa kunako Bongo Fleva, Faustina Charles au Nandy; ngoma inayokwenda kwa jina la Wasikudanganye.
Pia ndiye mwandishi wa ngoma ya wapenzi zilipendwa, Vanessa na Jux inayokwenda kwa jina la Unaniweza.
Mwamba huyu pia ametrendi na ngoma kali kama Unanikosha, Mama Amina, Wow, Tamu na nyingine kibao na kwa sasa anatamba na ngoma inayokwenda kwa jina la Beer Tamu.
IJUMAA SHOWBIZ imeanya mahojiano maalum (exclusive interview) na mtaalam huyo ambapo amefunguka mambo mengi ila kubwa zaidi ni sababu ya yeye kutoboa pua na kuvaa kipini;
IJUMAA SHOWBIZ: Mambo vipi Toto Badi, mzima wewe?
MARIOO: Niko salama kabisa Mungu ni mwema.
IJUMAA SHOWBIZ: Hongera kwa ngoma yako ya Beer Tamu tunaona inaendelea kufanya vizuri siku hadi siku…
MARIOO: Ahsante sana.
IJUMAA SHOWBIZ: Unazungumziaje mapokea ya ngoma yako hiyo?
MARIOO: Nashukuru sana Mungu kwa hilo ila pia shukrani nyingine ziende kwa mashabiki wangu maana bila wao mimi nisingekuwa hapa nilipo sasa.
IJUMAA SHOWBIZ: Kwenye kizazi hiki cha muziki sasa hivi unaweza ukajipa jina gani Marioo kutokana na mambo mazuri unayoyafanya kwenye muziki wako?
MARIOO: Kwenye kizazi kile cha Aslay, yeye ni Mfalme kwa mawazo yangu kwa sababu alitoka na Naenda Kusema kwa Mama na alitoka yeye mwenyewe akiwa mdogo, alinivutia sana kuona hata mimi naweza kufanya.
IJUMAA SHOWBIZ: Kwa hiyo kwenye kizazi hiki wewe unajipa jina gani?
MARIOO: Kwenye kizazi hiki mimi ndiye Mfalme, hiyo haipingwi kwa kuangalia namba kila mahali, idadi ya hit songs (ngoma kali), so mimi nastahili kuwa Mfalme wa kizazi hiki.
IJUMAA SHOWBIZ: Sawa ni mfalme na kwa levo uliyofikia Marioo unafanya shoo kuanzia bei gani?
MARIOO: Mimi sasa hivi sifanyi shoo chini ya milioni 20 na kwenda mbele. Chini ya hapo sifanyi.
IJUMAA SHOWBIZ: Kwa hiyo ikija pesa chini ya milioni 20 shoo hufanyi?
MARIOO: Inategemea na mazungumzo sasa kama tukielewana nafanya ndiyo maana sasa hivi kwenda kwenye shoo ndogondogo nimepunguza kabisa.
IJUMAA SHOWBIZ: Tukitoka kwenye masuala ya muziki kidogo, Marioo tunaona umekuja na mwonekano mwingine tena…
MARIOO: (anashanga) Mwonekano upi tena?
IJUMAA SHOWBIZ: Umeona kusuka rasta kichwani haitoshi, sasa umeamua kutoboa pua kabisa na kuvaa kipini?
MARIOO: Hiyo siyo nje ya muziki ni sehemu ya sanaa yangu kabisa.
IJUMAA SHOWBIZ: Je, unaona ni sahihi kwa mtoto wa kiume kutoga pua?
MARIOO: Ni sehemu ya muziki.
IJUMAA SHOWBIZ: Na ni nani aliyekushauri kufanya jambo kama hilo na huoni kama kwenye imani ya dini yako siyo sahihi?
MARIOO: Hakuna aliyeweza kunishauri. Ni mimi mwenyewe tu.
IJUMAA SHOWBIZ: Unaswali kweli Marioo?
MARIOO: Ndiyo, hakuna siku ambayo siswali.
IJUMAA SHOWBIZ: Unadhani kwa hicho ulichokifanya Mungu anaweza kupokea dua zako?
MARIOO: Kwa kweli tuachane na hilo kwa sababu hii ni sanaa ndiyo inatufanya kuwa hivi.
IJUMAA SHOWBIZ: Mbona ulivyokuwa hujatoga ulipendeza na kuvutia mashabiki wako tu?
MARIOO: Naomba tuachane na jambo hilo tafadhali.
IJUMAA SHOWBIZ: Kwa stahili hiyo huoni kwamba unaweza kupoteza mashabiki?
MARIOO: Mashabiki pia wanaelewa kuwa yote haya ni kwa ajili ya sanaa na siyo vitu vingine.
IJUMAA SHOWBIZ: Komenti zimekuwa nyingi juu yako wameanza kukuhusisha kwenye mambo mabaya (ushoga), hebu waambie kitu kidogo mashabiki wako…
MARIOO: Sipendezwi kabisa na maneno ambayo wananiambia mimi huko mitandaoni maana mimi siyo mtu wa hivyo kabisa; yaani najiheshimu sana hii ni sehemu ya sanaa tu.
IJUMAA SHOWBIZ: Tukirudi kwenye muziki tunaona kwa wasanii wengi wanarudisha kwa jamii, wewe vipi mipango yako?
MARIOO: Hata mimi pia ninafikiria sana juu ya jambo hilo kwa sababu ni zuri sana.
IJUMAA SHOWBIZ: Unatarajia kufanya nini?
MARIOO: Natamani sana kurudisha hata kwa kufungua gereji ambazo zitakuwa ni sehemu ya ajira kwa vijana ambao wapo mtaani (hata yeye alikuwa ni fundi kwenye gereji).
IJUMAA SHOWBIZ: Kwa nini gereji na siyo kitu kingine?
MARIOO: Kwa sababu ni kazi nzuri endapo mtu akiifanya kwa mahaba (passion). Kazi ya ufundi wa magari usichukulie kama kazi ya mtu aliyekosa malengo, hapana, ni kazi kama kazi nyingine hata mimi kabla ya hapa nilikuwa ni mshika spana mzuri sana.
IJUMAA SHOWBIZ: Unatarajia kufanya lini jambo hilo?
MARIOO: Siku ikifika nitaweka wazi.
IJUMAA SHOWBIZ: Ahsante sana na nashukuru kwa ushirikiano wako Marioo.
MARIOO: Ahsante pia na karibu tena.
MAKALA: KHADIJA BAKARI, BONGO