MWENYEKITI wa Chama wa Wamiliki wa Malori Wadogo na Wa Kati, Chuki Shabani, (kushoto) akitoa shukrani kwa Raisi Samia Suluhu kwa kuwasaidia changamoto yao. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Mark Gama.
WAMILIKI malori wadogo na wakati nchini, wametoa pongezi zao za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Raisi Suluhu Hassan kwa kuwatatulia changamoto ya kuzuiliwa kwa malori yao yaliyobeba magogo nchini Zambia ambayo yalikuwa yakitokea nchini, Congo DR

Akizungumza na wanahabari Dar, leo Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki Wadogo na wa Kati wa Malori nchini, Chuki Shabani amesema baada ya malori yao zaidi ya 400 kushikiliwa kwa zaidi ya miezi minne nchini Zambia walijaribu kutafuta ufumbuzi wa aina mbalimbali bila mafanikio lakini suala hilo lililopofika kwa Raisi Samia mara moja alilifanyia kazi na malori yao yaliyokuwa yameshikiliwa nchini humo yalianza kuachiwa na kuanza safari ya kurudi nchini, Tanzania.

Hata hivyo Chuki amesema licha ya malori hayo kuanza kuachiwa yalipofika eneo la Push nchini humo yalikamatwa tena na askari wengine waliodai hawajapewa idadi ya malori yaliyotakiwa kupita eneo hilo.

Askari hao wamewataka madereva hao kusubiri eneo hilo mpaka watakapopewa idadi ya malori yanayotakiwa kupita eneo hilo na mamlaka ya mapato ya nchi hiyo, ZRA.

Hata hivyo wamiliki hao wanaendelea kumuomba Raisi Mama Samia aendelee kuwapambania ili kumaliza kabisa changamoto hiyo ya madereva hao waliozuiliwa tena eneo hilo ambalo imedaiwa kuwa ni porini na hapana huduma za kibinaadamu kama vile maji, vyoo, vyakula na mengineyo.
Wamiliki hao wameiomba serikali ya Raisi Mama Samia kutengeneza njia nyingine ya kutokea nchini DRC Congo bila kupitia Zambia ambapo wamesema wamechoshwa na visa mbalimbali visivyoisha wanavyofanyiwa wanapopita nchini hapo.
Akijibu swali la wanahabari kuhusu kifuta jasho kwa madereva hao walioteseka na malori hayo kwa miezi minne waliyoshikiliwa, mmiliki wa malori, Peter Kirigini amesema kwa kipindi chote madereva hao walipokuwa kizuizini nchini humo walikuwa wakihakikisha wanapata huduma zote za msingi ikiwemo vyakula, matibabu na nyinginezo.
Kirigini ameongeza kuwa si huduma hizo tu bali mpaka mishahara yao walikuwa wakiwapatia kama kawaida licha ya wao wamiliki wa malori hayo kutoingiza chochote kutokana na magari yao kutofanyakazi na kuingiza chochote.
“Sisi wamiliki ndiyo tunaumia zaidi kwakuwa magari yetu yalikuwa hayaingizi chochote kwa kipindi chote hicho lakini sisi tumekuwa tuwakigharamia kila kitu madereva wetu maana tunajua posho ya safari ilishawaishia muda mrefu.
Na katika hili wamiliki na madereva hakuna wa kumlaumu mwenzake kwakuwa wote ni wahanga wa hili tatizo na hakuna aliyetarajiwa kutokea janga hili hivyo cha msingi ni kuangalia masuala ya ubinaadamu tu,” alimaliza kusema Kirigini.
Naye Mgendela Gama mmoja wa wamiliki hao aliendelea kumpongeza Raisi Samia kwa kulifanyia kazi kiukaribu suala lao na kuzidi kumuomba aendelee kulisimamia mpaka madereva wao wote wasio na hatia wafike salama hapa nchini.
HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS /GPL