
MBUNGE wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo, amekabidhi Magodoro 70 yenye thamani ya Sh milioni tatu kwa ajili ya wanafunzi Shule ya Sekondari Nyehunge iliyoko Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema baada ya moto kuteketeza mabweni na vifaa vya wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita katika shule hiyo.
Akikabidhi Magodoro hayo, Katibu wa Mbunge huyo, Butogwa Masalu, amesema Shigongo ameona ni vema kujitolea alichonacho ili kuwasaidia wanafunzi hao ambao vifaa vyao viliteketea kwa moto baada ya bweni kuungua.

Amewataka wadau wengine kujitokeza kuongeza nguvu ili kuwasaidia watoto hao waweze kupata mahala pa kujistiri.
“Shigongo ameguswa na Jambo hili ambalo lilitokea kutokana na janga la moto, magodoro haya yatawasaidia watoto hawa ili waweze kutulia na kusoma kwa utulivu,” amesema Butogwa.
Mabweni ya Shule ya Sekondari Nyehunge yaliteketea kwa moto katika tukio lilitokea Septemba 27 na Septemba 29 mwaka huu ambapo chanzo chake hadi sasa hakijafahamika.

Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Buchosa, Bruno Sangwa amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Buchosa Eric Shigongo kwa kutoa msaada huo ambao utasaidia wanafunzi hao.
Amesema kujitoa kunahitaji moyo na amewaomba wadau wengine waweze kujitokeza kusaidia kwani mahitaji bado yanahitajika.
Katika tukio hilo la moto, wanafunzi wapatao 161, magodoro yao yaliteketea kwa moto kati ya wanafunzi 286 wa kidato cha Tano na Sita kwenye shule hiyo.

Diwani wa Kata ya Nyehunge, Kulwa Shindika amewataka walimu kusimamia nidhamu kwa wanafunzi wa shule hiyo ili kuepuka majanga ya moto kujitokeza katika shule hiyo.
Sambamba na walimu amewataka pia wanafunzi kuzingatia masomo yao na kuacha masuala yasiyofaa ili watimize ndoto zao.
Mmoja wa mwanafunzi ambaye vifaa vyake viliteketea kwa moto, Rahimu Ayubu anayesoma kidato cha Sita, amesema wanashukuru kwa msaada waliopata kutoka kwa Mbunge.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Nyehunge waliounguliwa vifaa vyao kutokana na Mabweni yao kuteketezwa kwa moto wamemshukuru Mbunge wa Jimbo la Buchosa Eric Shigongo kwa msaada wa magodoro 70 ambayo yatawasaidia.