
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa ukorofi na kukosekana kwa nidhamu ndiyo kulikopelekea kumhamisha tena kwa kumhurumia aliyekuwa Mkurugenzi wa wilaya ya Longido Juma Mhina, ili akajifunze.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Oktoba 18, 2021, wakati akizungumza na wananchi wa Longido, ambapo amewasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa nidhamu na kusema kwamba asingemhurumia asingemteua tena.
“Longido hapa kulikuwa na Mkurugenzi mkorofi sana, hakukuwa na nidhamu ya kufanya kazi ndiyo maana nikamtoa nikampeleka sehemu nyingine akajifunze na hilo ni kumhurumia ilikuwa nimuache kabisa,”- Rais Samia Suluhu Hassan.
Mbali na hayo, Rais Samia amewataka wananchi wa Namanga kuendele kuwa na uvumilivu katika kulifanya eneo hilo kuwa Mji na kwamba bado halijakidhi vigezo.
“Mnataka Namanga iwe Mji Mdogo lakini tukiitoa Namanga kuifanya Mji Mdogo mnaiua Longido, tusubirini tuongeze vyanzo vya mapato maendeleo yaonekane halafu tutafikiria hayo mambo baadaye lakini kwa sasa naomba mbaki kama mlivyo,” Rais Samia
Rais Samia bado anaendelea na ziara yake ya kikazi mikoa ya Kaskazini ambapo alianza na Mkoa wa Kilimanjaro siku ya Ijumaa na sasa yupo mkoani Arusha.