×

Harusi ya Mtoto wa Bilionea, Mastaa Wafunika -Video

Siku kadhaa zilizopita, picha za wanandoa na mastaa wakubwa duniani, Jay Zee na Beyonce zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, zikiwaonesha wakiwa Venice nchini Italia, ambako ilielezwa kwamba wanakwenda kuhudhuria kwenye sherehe ya harusi iliyokuwa inafanyika nchini humo.

 

Baadaye, zikasambaa picha za mastaa wengine, Pharrel Williams na Kanye West, wote wakiwa nchini Italia ambao nao ilielezwa kwamba wanakwenda kuhudhuria harusi hiyo na baadaye, video zinazomuonesha Kanye West akitumbuiza kwenye harusi hiyo, nazo zikashika kasi mitandaoni.

 

Maswali yakawa mengi, ni harusi gani inayoweza kuwakutanisha mastaa wakubwa kiasi hicho duniani? Ni nani aliyekuwa anafunga ndoa? Makala haya yatakupa majibu ya maswali yote uliyokuwa ukijiuliza.

 

Hiyo ilikuwa ni harusi ya Alexandre Arnault ambaye alikuwa akifunga ndoa na mwanadada mrembo, Geraldine Guyot. Pengine sasa utakuwa na shauku ya kutaka kujua, Alexandre Arnault ni nani mpaka harusi yake ihudhuriwe na mastaa wakubwa kiasi hicho?

 

Alexandre ni mtoto wa pili kati ya watoto watano wa mfanyabiashara mkubwa duniani na mmiliki na CEO wa Kampuni ya Moët Hennessy Louis Vuitton (MHLV), Bernard Arnault ambaye kwa sasa, anashika nafasi ya tatu kati ya mabilionea wakubwa zaidi duniani.

 

Ukimtoa bilionea wa kwanza duniani kwa sasa, Jeff Bezos na bilionea wa pili, Elon Musk, wa tatu ndiyo huyu Bernard Arnault. Miezi michache iliyopita, Mei 2021, Arnault alitangazwa kuwa ndiye bilionea namba moja duniani lakini haukupita muda mrefu akazidiwa na Jeff Bezos na Elon Musk na kumfanya ashike nafasi ya tatu!

 

Bila shaka sasa umeanza kupata picha! Ilikuwa ni harusi ya mtoto wa bilionea wa tatu duniani na ndiyo maana mastaa wakubwa kama Jay Z, Beyonce na wengineo, walifurika kwa wingi huku mtumbuizaji mkuu akiwa ni Kanye West ambaye aliperform mbele ya maharusi hao.

 

Hii ni mara ya pili kwa Alexandre na mkewe kufanya sherehe ya harusi, miezi mitatu iliyopita, walifunga ndoa rasmi jijini Paris na kufanya sherehe ya kifahari ambayo hata hivyo, ilihudhuriwa na watu wachache tu, wageni waalikwa ambao wengi kati yao, walikuwa ni mabilionea.

 

Kwa upande wa bibi harusi, Géraldine Guyot mwenye asili ya Ufaransa, naye mambo yake si mchezo. Huyu ndiye mmiliki wa lebo kubwa ya mavazi na vito vya thamani ya D’Estrëe ambayo ni miongoni mwa brand kubwa nchini Ufaransa na duniano kote, ikijikita katika ubunifu wa mavazi ya kike pamoja na vito vya thamani na anatajwa kuwa shabiki mkubwa wa Beyonce.

 

Mwaka 2020, mwanadada huyu alitajwa na Jarida la Forbes katika orodha ya wanawake 30 waliokuwa wakifanya vizuri zaidi duniani katika biashara ya vito vya thamani na urembo wa wanawake mitandaoni.

 

Wawili hawa walikutana Paris, Ufaransa mwaka 2019 na kuangukia penzini ambapo baadaye walivishana pete ya uchumba na hatimaye kuoana.

 

Alexandre mwenye umri wa miaka 29, ndiye makamu mwenyekiti wa Kampuni ya Tiffany ambayo pia inamilikiwa na baba yake na kabla ya hapo, alikuwa mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza mabegi ya kisasa ya Rimowa na Kampuni ya Ubunifu wa Mavazi ya Fendi, ambazo zote zinamilikiwa na familia hiyo .

 

Nje ya biashara za familia, Alexandre ni mhandisi ambaye alisomea nchini Ufaransa katika Vyuo vya Ecole Telecom ParisTech na Ecole Polytechnique. Baada ya kuhitimu masomo yake, amewahi kufanya kazi katika kampuni za McKinsey na KKR.

 

Miongoni mwa biashara zilizompatia utajiri mkubwa baba wa bwana harusi, Bernard Arnault ni pamoja na biashara za brand kubwa za mavazi na pafyumu duniani zikiwemo Christian Dior, Fendi na Louis Vuitton sambamba na utengenezaji wa shampeni za Moët Hennessy zinazotajwa kuwa miongoni mwa vinywaji vinavyouzwa bei ghali zaidi duniani.

 

Pia anatajwa kumiliki brand nyingine za mavazi, pafyumu na vipodozi kwa kushirikiana na watu wengine, zikiwemo Supreme, Givenchy, Marc Jacobs, Belmond na Fenty.

 

Bilionea huyo pia anatajwa kuwa miongoni mwa mabosi wa platform kubwa ya filamu duniani ya Netflix tangu mwaka 1999 huku pia akijihusisha na biashara ya kukodisha boti za kifahari zikiwemo Princess Yachts, Symphony na nyingine nyingi.

 

Familia yake inaishi katika jumba la kifahari lililopo Saint-Emilion, Bordeaux nchini Ufaransa na inaelezwa kuwa pia familia hiyo inamiliki kisiwa kimoja huko Bahamas kiitwacho Indigo Island pamoja na ndege ya kusafiria, Private Jet!

 

Leave a Comment