×

Mwonekano wa Mondi Kama Rapa Rick Ross

MIONGONI mwa mambo yaliyozua minong’ono pale Mlimani City jijini Dar, wikiendi iliyopita wakati staa wa muziki Afrika, Diamond Platnumz akizindua kampuni yake ya michezo ya kubahatisha, ni pamoja na mwonekano wa jamaa huyo.

 

Diamond aliwachanganya kwenye mwonekano mpya ambao ameanza kudunduliza ndevu ili kupata mwonekano kama wa Rapa wa Marekani, Rich Ross ambaye hivi karibuni amekuwa gumzo Bongo kutokana na ukaribu wake na mwanamitindo wa Tanzania, Hamisa Mobeto; wengine wanadai ni wapenzi.

 

Awali, Diamond alikuwa na vindevu vidogo kwa chini; wengine wanaita vimzuzu, lakini sasa anapalilia nduvu za mashavuni kama Rick Ross ambaye aliwahi kufanya naye wimbo unaokwenda kwa jina la Waka.

Ikumbukwe kwamba, Hamisa amezaa mtoto mmoja wa kiume na Diamond aitwaye Dyllan.

 

Watu wanasema, Diamond au Mondi ameanza kufuga ndevu hizo baada ya kuwepo kwa stori nyingi mitandaoni juu ya Hamisa na Rick Ross kwani kabla ya hapo hakuwa nazo.

 

Hata hivyo, baadhi ya watu waliomshuhudia Diamond uso kwa uso na ambao hawakuwa wamemuona hadharani zaidi ya mitandaoni na kwenye video za nyimbo zake walikuwa na maoni tofauti huku Hamisa akiangushiwa jumba bovu kuwa huwenda ukaribu wake na Rick Ross ndiyo umesababisha jamaa huyo naye afuge ndevu.

 

Hata hivyo, swali lililokosa jibu ni juu ya ni kwa namba gani Hamisa anahusika ilihali inafahamika yeye na Diamond si wapenzi na hata enzi za penzi lao, mwanamama huyo alikuwa ni mchepuko kwani jamaa huyo alikuwa kwenye mapenzi na Zari.

 

“Anadhani akifuga ndevu atamvutia Hamisa amtose Rick Ross arudi kwa Mama Dangote na Esma wakashikane uchawi vizuri.

“Labda Diamond amejua sababu ya kukimbiwa na Hamisa ni hizo ndevu, lakini kama anataka afanane na Rick Ross inabidi aongeze na mwili pia.

 

“Ni kweli Hamisa ameshasema anampenda Rick Ross kwa sababu ya hizo ndevu nyingi mashavuni, meno yake meupe na anavyonukia kwa hiyo huwezi kujua, labda Diamond anataka kuwa na vigezo hivyo ili naye aitwe Daddy kama Rick Ross anavyoitwa na Hamisa,” alisema mmoja wa mashambenga wa mastaa.

 

Hata hivyo, kwa upande wake, Hamisa amekuwa akikanusha kwamba amekuwa akionekana na Rick Ross ili kumkomoa Diamond.

Mama huyo wa watoto wawili anasema kuwa huwa hafuatilii maisha ya wapenzi wake wa zamani wala kujali kuhusu wanawake watakaochumbia baada yake.

Anasema huwa hana kinyongo chochote dhidi ya mpenzi wake yeyote wa zamani.

“Mimi ni mpenzi wa zamani asiye na matatizo. Mimi ni ex ambaye siwezi kujali kuhusu kile unachofanya sasa hivi.

 

“Huwa najali cha kwangu kwa muda wangu. Ikitokea kwamba tumeachana, hayo yameisha. Siwezi kujali ukiwa na mwanamke mwingine na sidhani kama nimewahi kujali kwa ex wangu yeyote akiwa na mwanamke mwingine. Naamini kwamba kila kitu kinatokea kwa sababu ni chema, kitu kikija kwako ni cha kwako. Kama siyo cha kwako basi siyo cha kwako.

 

“Pia naamini watu huchumbiana na kuachana, mkiachana inamaanisha riziki inaishia hapo ama Mwenyezi Mungu alitaka ufike hapo uendelee na safari. Mimi sijawahi wazia ex wangu yeyote yule vibaya. Sijawahi kufanya kitu kwa ajili ya yeyote yule. Huwa nafanya mambo yangu na kufanya yale yanayonifurahisha,” anasema Hamisa.

 

Hata hivyo, pamoja na maneno mengi, lakini baadhi ya mashabiki wanamsifia Diamond kwamba mwonekano huo wa kufuga ndevu na kuwa na msitu mashavuni kama Rick Ross au Mpoki kama Wabongo wengi wanavyomuita, unampendeza huku wengine wakimfananisha na rapa Drake na wengine wakimfananisha na Benard Morrison wa Simba.

STORI; SIFAEL PAUL, DAR

Leave a Comment