
Mkutano wa tano wa bunge la 12 unatarajia vikao vyake huku miongoni mwa shughuli zitakazofanyika ni pamoja na wabunge kujadili na kuishauri Serikali kuhusu mapendekezo ya utekelezaji wa mpango wa taifa kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge ya 94(1), katika mkutano wake wa Oktoba-Novemba kwa kila mwaka, Bunge kwa siku zisizopungua tano litakaa kama Kamati ya Mipango ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 63(3)(C) ya Katiba kwa kujadili na kuishauri serikali kuhusu mapendekezo hayo.
Katika mkutano huo, Bunge pamoja na mambo mengine litapokea, kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali.
Aidha, kwa mujibu wa kanuni ya 94 (2) (b) pia Bunge litapokea, kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu vyanzo vya mapato vya serikali na (C) litapokea, kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu mapendekezo ya utekelezaji wa mpango wa serikali na vipaumbele kuhusu mpango huo.
Ratiba inaonyesha kuwa wabunge watapokea maelezo kuhusu maeneo ya vipaumbele vya matumizi ya fedha za mkopo nafuu zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwa ajili ya kukabiliana na athari za Uviko-19.
Pia Bunge litapokea maelezo kuhusu miradi ya nishati ya umeme ya kimkakati na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wake na taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo.