×

Video Zikionyesha Sabaya Akipewa Mamilioni Benki Zatua Mahakamani

VIDEO sita zilizokuwa kwenye ‘flash’ zimepokewa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi kwenye kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, huku watu wawili wakionekana kuingia ndani ya benki wakitoa na kuchukua maburungutu ya fedha ambazo ziliwekwa kwenye boksi.

 

Flash hiyo, iliwasilishwa mahakamani na shahidi wa nane wa Jamhuri, Johnson Kisaka (35), kama kielelezo cha ushahidi.

 

Sabaya na wenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, wakikabiliwa na mashtaka matano ya uhujumu uchumi. Washtakiwa wengine ni Sylvester Nyegu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), Jackson Macha (29) na Nathan Msuya.

 

Video hiyo ilionyesha watu hao wawili wakiingia katika benki hiyo, Januari 22 majira ya 10:10 na kutoka saa 11:03 na baada ya kutoka na hela hizo waliingia nazo kwenye gari lenye rangi ya bluu.

 

Wakati huo, ofisa wa benki hiyo alifika katika eneo la mapokezi “Kaunta” akiwa ameshika boksi mkononi na kuanza kuzipangilia fedha ndani ya boksi hilo na baada ya kukamilisha mchakato wa kuhakiki fedha hizo, aliziweka juu ya kiti cha kuzunguka na kupeleka kuwakabidhi wahusika.

 

Watu hao walitoka kwenye benki hiyo wakiwa wamebeba boksi hilo kwa pamoja. Kadhalika watu hao, mmoja akiwa mtu wa makamo, alivaa koti kubwa kama mtu anayefanya kazi gereji huku mwenzake akiwa ni kijana.

 

Wakati mchakato mzima ukiendelea wa kusubiri fedha kutolewa benki, kijana huyo alikuwa akiimarisha ulinzi huku akizunguka benki na kumfuata nyuma mzee kila sehemu alipokuwa anakwenda na baada ya kuchukua maburungutu ya fedha hizo, waliondoka pamoja.

 

Pia video hiyo ilionyesha kijana huyo akiwa amevaa fulana ya mistari, kofia nyeusi na suruali nyeusi. Shahidi huyo, alidai video za CCTV kwenye Benki ya CRDB zilitolewa tawi la kwa Morombo, jijini Arusha.

Alidai baada ya kutoa ushahidi huo, alimkabidhi Ramadhani Juma ambaye ni Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

 

PINGAMIZI LATUPWA

Awali, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, inayosikiliza kesi hiyo chini ya Hakimu Mkazi, Pastricia Kisinda, ilitupilia mbali pingamizi la mawakili wa utetezi, juu ya kupokewa mahakamani kwa flash yenye video sita.

 

Akitoa uamuzi mdogo kuhusu pingamizi hilo, Hakimu Kisinda alisema baada ya mahakama kupitia kifungu cha 64A cha Sheria ya Ushahidi Namba 6 ya mwaka 2019 na kifungu cha 18(1), (2) cha Sheria Kielektroniki namba 13 ya mwaka 2015, vielelezo hivyo vimekidhi vigezo vya kupokewa.

 

Oktoba 28, mwaka huu, mawakili wa utetezi walipinga kupokewa kwa flash ambayo ndani imewekwa video sita kama kielelezo cha ushahidi kwa madai kuwa hazikuonyeshwa kabla ya kukubaliwa kupokewa.

 

Pingamizi hilo liliwasilishwa na Wakili wa Utetezi, Mosses Mahuna, kabla ya kuwasilishwa na shahidi wa nane wa Jamhuri, Jonson Kisaka (35), ambaye ni ofisa wa maabara ya uchunguzi wa kielektroniki kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

 

Nyaraka nyingine zilizopingwa kupokewa kama vielelezo vya ushahidi na mawakili hao ni fomu namba 28 na 29 pamoja.

 

Katika pingamizi hilo, Mahuna alidai kuwa vielelezo hivyo ikiwamo flash, shahidi huyo alifungua ripoti mwanzoni bila kucheza video sita zilizopo ndani yake. Mahuna alidai kwamba sheria inaelekeza wanapotoa vielelezo vinatakiwa kupitiwa au kufungua video hizo ili kutambua ni kitu gani kimewekwa.

 

Pia alidai kwamba sheria imeelekeza na inataka kupatiwa kielelezo hicho kwa mapana yake ili kutambua ni kitu gani kimo ndani ya kifaa hicho.

 

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Filex Kwetukia, alidai utaratibu wa kisheria wa kuwasilisha vielelezo hivyo umezingatiwa kwa kuwa shahidi ameonyesha vitu ambavyo amevizungumzia wakati akitoa ushahidi wake wa msingi.

 

Alidai kuwa Sheria ya Kielektroniki kifungu cha 15 hakijaeleza kuwa kielelezo kinatakiwa kusomwa ndipo kipokewe mahakamani.

 

Naye Othmed Mtenga, Wakili wa Serikali Mwandamizi, aliiomba mahakama kupokea flash hiyo na nyaraka nyingine kwa kuwa wamefuata utaratibu wa kisheria.

 

Alidai kuwa hoja hizo haizuii flash na nyaraka kupokewa kwa kuwa kinachoangaliwa ni kama shahidi anautambua ushahidi anaouzungumzia na kama amehusika kuuandaa. Pia alidai kisheria shahidi anatakiwa kuelezea kielelezo hicho kabla ya kukitoa mahakamani.

 

“Tunaiomba mahakama kupokea kielelezo hiki kwa kuwa shahidi ameeleza kwamba anakifahamu. Pia hoja ya kusema kielelezo kionyeshwe nini kilichomo ndani ni sawa na kukifungua kabla ya kupokewa kwanza kwa kuwa kiutaratibu unatakiwa kupokelewa ndipo kisomwe mahakamani,” alidai.

Leave a Comment