
KATIKA hali ya kushangaza, mwanamasumbwi wa uzito wa Super Bantam nchini Zimbabwe, Taurai Zimunya Samson (24), amefariki dunia siku ya Jumatatu ya wiki hii, baada ya kuzimia kutokana na kichapo wakati wa pambano lisilo la ubingwa alilopigana siku ya Jumamosi iliyopita jijini Harare.
Hii ni mara ya kwanza kwa bondia kufariki nchini Zimbabwe kutokana na majeraha aliyoyapata ulingoni. Tukio hili limeibua maswali mengi huku Katibu Mkuu wa Bodi ya Kitaifa ya Kudhibiti Ndondi na Mieleka ya Zimbabwe (ZNBWCB), Lawrence Zimbudzana akisema kuwa uchunguzi kuhusu tukio hilo bado haujakamilika ili kufahamu zaidi chanzo cha kifo cha bondia huyo.
“Kwa sasa tunashughulikia taratibu za mazishi, na kisha tuketi na kuangalia nini kilisababisha kifo chake,” Zimbudzana alisema katika mazishi ya Zimunya yaliyofanyika jana Jumatano.
Taarifa iliyotolewa na ZNBWCB ilisema kuwa taratibu zote muhimu za matibabu zilifuatwa na msaada wa dharura wa matibabu ulitolewa mahali hapo kabla ya kupelekwa hospitali. Zimunya alipigwa makonde kadhaa kichwani katika raundi ya tatu ya pambano hilo la raundi sita. Aliyekuwa mkufunzi wake Tatenda Gada alihuzunika, akisema nyota huyo alikuwa na uwezo mkubwa.
“Tumeondokewa na hazina kubwa ya taifa katika fani ya masumbwi, Nilifanya kazi na Taurai kwa zaidi ya miaka minne nilimtazama akistawi na alikuwa mmoja wa nyota wajao katika fani hii,” Gada alisema.
Baba yake Zimunya, Samson, alikuwa bondia mahiri asiye wa kulipwa na alitarajia mtoto wake angebeba jina la ukoo na kuwa bingwa. Mashindano ya masumbwi nchini Zimbabwe yamerejea hivi karibuni baada ya vizuizi vya kupambana na janga la corona kulegezwa.