×

Kocha Mpya Simba Abakisha Siku 14

WAKATI Ligi Kuu Bara ikiwa imesimama kwa takribani wiki mbili, Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, imepanga kutumia muda huo kushusha kocha mpya wa kuinoa timu hiyo ambayo pia inajiandaa na mchezo wa Kombe la
Shirikisho Afrika dhidi ya Red
Arrows ya Zambia.

 

Novemba 28, mwaka huu, Simba itavaana na Red Arrows kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, ukiwa mchezo wa kwanza wa mtoano kusaka nafasi ya kwenda makundi ya michuano
hiyo, kabla ya kurudiana
Desemba 5, nchini Zambia.

 

Jina la Kocha Mkuu wa Horoya AC ya Guinea, Lamine N’diaye, ndiyo linalotajwa kumrithi aliyekuwa kocha wa
timu hiyo, Mfaransa, Didier
Gomes.


Akizungumza na
Spoti Xtra, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya timu hiyo, Asha Baraka, alisema kuwa bodi imepanga kumleta kocha huyo kabla ya mchezo huo wa kimataifa.


Kiongozi huyo alisema kuwa,
kocha huyo huenda akakaa katika benchi kwenye mchezo huo ambao timu hiyo watahitaji ushindi.


Aliongeza kuwa wajumbe wa
bodi wanatarajiwa kukutana kufanya kikao baada ya mchezo wa leo (jana) wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo FC.


“Ngumu kumleta kocha mpya
bila ya maamuzi ya pamoja ya wajumbe kukubaliana kwa pamoja baada ya kupitia CV za makocha kumi waliopitishwa katika mchujo wa awali.


“Mchujo wa mwisho
umepangwa kufanywa haraka mara baada ya mchezo wa ligi dhidi ya Namungo tutakaocheza
leo (jana).


“Baada ya mchujo huo
kufanyika haraka kocha mpya atatangazwa sambamba na kuanza kazi katika kipindi hichi
ambacho ligi imesimama,”
alisema Baraka.

STORI: WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA

Leave a Comment