
Mahakama Kuu ya Tanzania Divesheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi inatarajia kesho imepanga kutoa Uamuzi mdogo wa pingamizi lililowasilishwa na Mawakili wa Upande wa Utetezi katika kesi ya uhujumu Uchumi yenye Mashtaka ya Ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala umewasilisha pingamizi mbele ya Jaji Joachim Tiganga wakati wa shahidi wa nane wa upande wa Jamuhuri ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru, SP Jumanne Malangahe akitoa Ushahidi wake Mahakamani hapo wa namna alivyowapekuwa watuhumiwa Adam Kasekwa maarufu Adamoo na Mohamed Lingwenya eneo la Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya kukamatwa.
Katika hoja zao mawakili wa Utetezi akiwemo Nashon Nkungu na wenzake wanapinga kupokelewa kwa hati ya ukamataji mali ya Shahidi wa nane kama kielelezo cha Ushahidi kwa upande wa Jamhuri kwa madai kimekiuka matakwa ya Kisheria.
Pingamizi hilo linadai kuwa nyaraka hiyo imeandaliwa chini ya kifungu cha 38( 3) ya mwaka 1985 sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2018 sheria inayodaiwa kuwa haijawahi kufanyiwa mabadiliko mwaka huu wanaodai bali ilifanyiwa marekebisho 2019 hivyo haiwezi kuendana na sheria za nchi.
Upande wa utetezi umedai kuwa sheria hiyo waliotumia inafanya nyaraka hiyo kukosa nguvu ya kupokelewa mahakani hapo kwani haijulikani hivyo wanaomba mahakama isipokee kama kielelezo cha Upande wa Jamhuri.
Akijibu hoja hizo wakili wa serikali mwandamizi Robert Kidando, amedai kifungu namba 20 (1) a, b, c cha tafsiri ya sheria sura ya kwanza ya mwaka 2019 ,sheria hiyo ipo hivyo haiwezi kusemwa kwamba nyaraka hiyo imetengenezwa katika sheria ambayo haipo.
Kidando amedai katika mwaka 2018 kuna vifungu vya sheria ya CPA vilivyofanyiwa marekebisho ikiwemo mwongozo namba 7 wa mwaka 2018 ingawa haihusiani na kifungu 38 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Amedai katika mazingira hayo hawawezi kusema kwamba sheria hiyo haipo katika vitabu vya sheria, hoja hiyo haipo, na kuna CPA moja tu nchini na sura 20 moja tu Tanzania bara, hata katika kesi walizozirejea haziendani na mazingira ya kesi hiyo.
Amedai hatua waliyofikia ni kuona kama mahakama inaweza kupokea nyaraka hiyo na hakuna wakili hata mmoja kati yao anayelalamikia kama kulikuwa na ukiukwaji wa sheria wakati wa upatikanaji wa nyaraka hiyo.
Wakili Kidando amedai kuwa sheria inayoongoza upokelewaji wa ushahidi mahakamani zipo wazi ikiwemo uhalali wa shahidi, nyaraka hiyo pia imerejea kifungu cha 35 sheria ya polisi inayompa askari Mamlaka ya kufanya upekuzi, hivyo wanaomba mapingamizi ya upande wa utetezi yatupiliwe mbali na nyaraka hiyo ipokelewe.
Baada ya hoja za pande zote mbili shauri hilo limeahirishwa hadi kesho Novemba 9, mwaka huu kwa ajili ya Jaji Kutoa uamuzi mdogo wa kwamba mahakama ipokee nyaraka hiyo kma kilelezo cha ushahidia au laa.
Awali Shahidi Jumanne wakati akitoa ushanidi wake Amedai kabla ya kuwapekua alitafuta mashahidi ambapo aliwapata wanawake wawili na kwenda nao aneo la tukio ambapo alianza kwa kujipekua yeye mwenyewe na kuwahakikishia mashuhuda kuwa hakuwa na kitu mwilini mwake na baadaye akaanza kumpekua Kasekwa ambaye alimkuta na silaha aina ya Bastola yenye namba A5340 pamoja na kete 58 za dawa zilizodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.
Amedai upekuzi huo uliendelea kwa mtuhumiwa Lingw’enya ambapo alikutwa na simu kubwa aina ya Tecno ambayo ilikuwa na laini ya Halotel na Airtel na kete 25 za dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya. Amefafanua kuwa baada ya upekuzi vitu vyote vilijazwa kwenye hati ya ukamataji mali na kisha kusainiwa na wote watuhumiwa, mashahidi huru pamoja na yeye.
Amedai vitu vyote hivyo alivyopata katika upekuzi alimkabidhi askari mwenzake aliyemtaja kwa jina la Goodluck. Baada ya maelezo hayo shahidi huyo aliweza kuitambua hati hiyo kulingana na vitu walivyojaza pamoja na saini walizoweka na mwishowe akaomba mahakama ipokee hati hiyo kama kielelezo katika mwenendo wa kesi hiyo na ndipo upande wa utetezi walipoibua pingamizi.