×

Magari Matano Yagongana Dar

AJALI mbaya imetokea usiku wa kuamkia leo Jumamosi, Novemba 13, 2021 katika maeneo ya Mbezi kwa Yusufu, Dar es Salaam baada ya magari matano kugongana.

 

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kwamba lori la mizigo (Semi – Trailer) lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Iringa lilianguka barabarani baada ya kugongana na gari dogo aina ya Land Cruiser.

 

Baadaye lori jingine ambalo lilikuwa likitokea Kibaha mkoani Pwani kuelekea Dar es Salaam ambapo dereva wake hakufahamu kama mbele yake kuna ajali, aliligonga lori lililokuwa limeanguka na kuharibika vibaya.

 

Muda mfupi baadaye kutokana na kadhia katike eneo hilo la ajali, magari mengine mawili aina ya Toyota Noah na Toyota IST nayo yaligongana na kuharibika vibaya.

 

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo anasimulia; “Ajali ya kwanza imesababishwa na uzembe wa dereva wa Land Cruiser ambaye aliingia barabarani bila tahadhari, lakini ajali ya pili imesababishwa na kukosekana kwa alama za kuonesha kuwa mbele kuna ajali. Dereva wa lori (lililoanguka mara ya kwanza) ameumia vibaya na kupelekwa Hospitali,” amesema Shuhuda huyo.

Leave a Comment