
MZEE wa Vikao almaarufu Aristotee amesimamisha Jiji la Dar baada ya kufunga ndoa ya aina yake iliyoudhuriwa na mastaa kibao kutoka Bongo, huku zawadi za kutisha zikimwagika.
Ndoa ya Aristotee na Emmy ilifungwa katika Kanisa la Elishadai Temple Church lililopo Boko jijini Dar, Jumamosi iliyopita huku sherehe ya kufa mtu ikafuata pale Sea Breeze.
Aristotee alijizolea umaarufu kupitia mitandao ya kijamii na sasa anaonekana kuwa kati ya wanafamilia wa familia kubwa na yenye ushawishi ya Wasafi ikiongozwa na Diamond Platnumz au Simba wa Tandale.
Hii haikuwa ndoa ya kawaida kama zile zilizozoeleka mtaani, kwani Mzee wa Vikao aliamua kwenda na chopa hadi kanisani akiwa na kipenzi chake kisha kufunga pingu za maisha.
Wajuzi wa mambo wameitaja harusi ya Aristotee kuwa ni mpamgo mkakati wa kuzima soo alilolileta Harmonize, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lina madai mazito, twende pamoja;
HARMONIZE AZUA SOO
Ikumbukwe Konde Boy Mjeshi amerudi kutoka Marekani hivi karibuni huku akitoa ya moyoni juu ya bosi wake wa zamani, Diampnd akianika yote aliyotendewa na familia mzima ya WCB, maneno yamekuwa mengi huku kila mmoja akisubiri nini Simba atakisema juu ya tuhuma hizo zito kutoka kwa Konde Boy.
Bila kupepesa, Harmonize mara baada ya kuwasili Bongo, alieleza yote yaliyomkuta akiwa WCB huku akionesha nia yake ya kujisafisha kwa kile alichodai kuwa ni kuchafuliwa na Diamond katika jamii ili aonekane ni mtu mbaya na asiye na fadhila.
Harmo pia alieleza sababu ya kutofautiana na Diamond huku akiweka wazi njia alizotumia kutafuta suluhu ikiwemo ile ya kuongea hadi na Mama Diamond, lakini akagonga mwamba.
Konde Boy amerudi nyumbani huku akichafua hali ya hewa, sasa dunia inasikiliza na kuamini alichokizungumza huku watu wakikaa mkao wa kula kusubiri majibu ya Diamond.
MACHAWA WAHAHA
Wiki iliyopita ilikuwa ngumu kidogo kwa machawa, kufuatia kauli ya Harmonize ambaye alianika maovu yanayofanywa na machawa aliodai kuwa wanatumwa na Diamond ili kumshusha kimuziki.
Aliwataja machawa kama Baba Levo na Juma Lokole; kubwa zaidi Hamis Shaban Taletale au Babu Tale naye akitupa dongo kwa machawa wawili ambao ni Baba Levo na Juma Lokole.
Kauli ya Babu Tale ilimfanya Chawa Pro Max almaarufu Baba Levo kuhaha na kuanza kumrushia maneno kupitia Instagram.
Machawa wameonekana kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi na kuupaisha muziki wa Bongo Fleva miaka ya hivi karibuni, huku nao wakiingiza pesa ndefu kupitia uchawa wao ambao unawaongezea umaarufu kila kukicha.
Kauli ya Babu Tale ni kama ilitaka kuhitimisha ufalme wa machawa Bongo hivyo muhaho ni lazima ungetokea, maana watu wanajenga, wanaoa na wengine wanamiliki magari kisa uchawa tu.
DIAMOND AZIMA SOO LA HARMO
Pengine harusi ya Aristotee ambaye anajinasibu waziwazi kuwa ni Chawa wa Diamond, haikupangwa kwa ukubwa ule kama ilivyofanyika, wajuzi wa mambo wanasema kuwa harusi ya Aristotee imetumika kimkakati ili Dunia isahau maneno aliyozungumza Harmonize.
Wajuzi wa mambo wanafika mbali na kueleza kuwa, ile helikopta aliyotumia Aristotee kumfikisha kanisani ni mpango mkakati wa kuzua mjadala mitandaoni ili watu waongelee helikopta na waachanae na Konde Boy Mjeshi.
Kubwa zaidi; Diamond au Mondi anakuja kuzima kila kitu kwa zawadi alizomtunza Aristotee ambazo ni kufuru.
Simba huyo wa Tandale ametoa zawadi zenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 180 ambapo Simba alitoa pesa taslim shilingi milioni 15 huku akitoa pesa milioni 15 kwenye mfumo wa cheki.
Hakuishia hapo alitoa zawadi ya kiwanja chenye thamani ya shilingi milioni 50 kilichopo Kigamboni jijini Dar huku sherehe za harusi iyo ikirushwa live kupitia Wasafi TV kwa saa 5 ambazo thamani yake inatajwa kufikia shilingi milioni 100.
Hii pengine inaweza kuwa ni harusi ya kifahari kuwahi kutokea Bongo kwa mwaka 2021, lakini inatajwa kubeba ajenda ya kumzima Harmonize.
STORI; BAKARI MAHUNDU, DAR