
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wakizindua wa Shule ya Msingi Museveni iliyopo Wilaya ya Chato, Mkoani Geita.
Shule ya Msingi Museveni iliyopo Chato, ina Madarasa 20, Jengo la utawala 1, Matundu ya vyoo 37, ofisi 2, Maktaba 1 na Nyumba za walimu na na ujenzi wa shule umekamilia kwa 100%, na itachukua wanafunzi wa awali na darasa la 1-7. Shule imesajiliwa kama shule ya kutwa na inayotumia mtaala wa Kiingereza.
Akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Rais Samia amesema; “Tunakushukuru Rais Museveni kwa kutenga muda wako wa kuja kutuona ndugu zako Watanzania, tunakushukuru kwa kuwa nasi tangu Novemba 27 hadi leo tuko hapa Chato tunakamilisha ziara hiyo.
“Uwepo wako unaleta hisia za safari yako ya mwisho wilayani hapa Julai 2019 ambapo ulipokelewa na Hayati Rais, Dk Magufuli ndipo ulipoahidi kujenga shule hii lakini kwa kudra za Mwenyezi Mungu mwenzetu hayupo kushuhudia yale mliyoyakusudia.
“Mhe. Rais Museveni tunakushukuru kwa kugharamia ujenzi wote wa shule hii, gharama zilizotumika hapa si ndogo ni $ 1.670m mpaka kukamilika kwake ungeweza kutumia fedha hizi kwa watu wa Uganda ila kwa upendo wako uliona wana-Chato wana uhitaji zaidi.
“Rais Museveni umethibitishia maana halisi ya kuwa ‘ukimpa binadamu samaki atamla kwa siku moja lakini ukimpa elimu ataitumia maisha yake yote’. Kazi hii tutaibeba Serikali, tutamalizia pale paliko bakia ili shule hii ifikie viwango vile ambavyo Marehemu (Dk. Magufuli) alivitarajia kufikisha.
“Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na TAMISEMI itaandaa utaratibu wa kuhakikisha uwepo wa watumishi, vitabu, vifaaa muhimu na fedha za uendeshaji ili Shule hii iweze kupokea wanafunzi ifikapo Januari 15, 2022.
“Shule hii (Museveni Priamry School) italeta manufaa yafuatayo: 1. Itaongeza fursa kwa wanafunzi wote kupata elimu kwani majengo yamezingatia wanafunzi wenye mahitaji maalum, 2. Itaimarisha utoaji wa elimu bora kwa uwepo wa miundombinu yote muhimu.
“Ikikupendeza shule hii ya Museveni ipate shule dada/kaka kule Uganda ili waweze kubadilishana uzoefu na kutembeleana….” -Rais Samia Suluhu Hassan.