
Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu amesema Serikali inapanga kuongeza mabasi ya Mwendokasi kwa awamu ya kwanza kutoka 210 yaliyopo sasa hadi 305 ifikapo Julai 2022 kwa awamu ya kwanza, na kuleta mabasi yapatayo 755 kwa ajili ya kutoa huduma kwenye awamu ya pili ifikapo Machi 2023.
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo jana wakati akielezea mafanikio, changamoto na mwelekeo wa TAMISEMI Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania ambapo amesema Serikali inaanza maandalizi ya kuongeza mabasi kwenye awamu nyingine hadi kufikia kiasi cha mabasi yapatayo 3,650 yanayohitajika kwa awamu zote ifikapo mwaka 2025.
“Tunapanga kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya mradi yenye jumla ya kilometa 109.74 ifikapo mwaka 2025, hii ikiwa ni kwa awamu zote sita kwa Mkoa wa Dar es Salaam sambamba kuanza kwenda kwenye miji mara baada ya maboresho ya kufanyika kwa sheria.
“Tutakamilisha ujenzi na usimikaji wa mfumo wa kielekroniki wa kukusanya nauli uliofungamishwa na Mfumo wa Kuongoza Magari (ITS) ifikapo Julai 2022, ikiwa ni sehemu endelevu ya maboresho ya huduma ya usafiri wa umma mijini….” amesema Ummy.