×

Rais Samia Acharuka, Avunja Bodi TPA, Shirika la Meli

Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumamosi Desemba 4,2021 wakati akizindua gati katika Bandari ya Dar es Salaam ametangaza kuzivunja Bodi ya Mamlaka ya Badari Tanzania (TPA) na ile ya Shirika la Meli kwa kuwaondoa wenyeviti wake baada ya kutoridhika na utendaji kazi wao.

 

Pia, ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi baada ya kunusa harufu ya ufisadi ikiwemo baadhi ya kampuni kulipwa fedha kwa ajili ya kutengeneza mifumo, lakini kazi haikufanyika.

Bodi ya Wakurugenzi wa Bandari inaundwa na mwenyekiti wake Profesa Ignas Rubaratuka huku Makamu wake akiwa Dk Delphine Magere. Wajumbe ni Malata Pascal, Dk Jabiri Bakari, Masanja Kadogosa, Jayne Nyimbo, Mhandisi Ephrem Kirenga na Eric Hamissi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Bandari.

Huku akionyesha kufahamu mambo mengi yanayoendelea ndani ya taasisi hizo, Rais Samia amesema kuna madudu mengi yanayofanywa ndani ya mamlaka hizo.

 

Amesema licha ya baadhi ya madudu hayo kuonyeshwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.

Rais Samia amesema bado kuna mianya ya uvujaji wa mapato katika mamlaka kutokana na mifumo ya malipo kuchezewa na wafanyakazi.

Leave a Comment